Michezo

EPL: Guardiola aomba Liverpool ijikwae ili aifikie

January 15th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

KOCHA wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini Uingereza Manchester City, Pep Guardiola amewaonya viongozi wa ligi hiyo Liverpool kwamba watatumia kujikwaa kwao katika mechi moja tu ili kuwafikia uongozini.

Liverpool wanaongoza msimamo wa jedwali la EPL na pana mwanya wa alama nne inayotamalaki kati yao na Manchester City.

Man City waliendelea kuipa Liverpool upinzani kileleni mwa msimamo wa jedwali la ligi baada ya kuwabamiza Wolvehampton Wanderers 3-0  usiku wa Jumatatu Januari 15.

Mshambulizi Gabriel Jesus alifunga mabao hayo mawili katika kipindi cha kwanza kabla ya mlinzi wa Wolves, Willy Bolly kujifunga mwenyewe katika kipindi cha pili.

Hata hivyo, Guardiola  alikataa kuzungumzia kwa kina ushindani ligini akisema atashughulika tu matokeo yanayosajiliwa na timu yake.

“Kile tunaweza ni kuzishinda mechi zetu. Nimezungumza na wachezaji wangu kuhusu ushindani huo na ukweli ni kwamba hatuna uwezo wa kudhibiti uchezaji wao katika mechi zao. Kile tunaweza kuomba ni wajikwae ila hilo lisipotendeka basi huenda watakuwa mabingwa.”

“Tumekuwa timu bora tangu msimu uliopita wa 2017/18 na msimu huu wa 2018/19 ingawa wamekuwa wazuri zaidi kutuliko ndio maana wapo katika nafasi ya pili,” akasema Guardiola.

Mabingwa hao wameanza mwaka huu kwa kishindo baada ya kumimina wavuni mabao 21 katika mechi zote nne za nyumbani na pia kushinda mechi yao ya Shirikishoi la soka nchini humo (FA).