Michezo

EPL: Ighalo asema wanajihisi wako tayari kikosini Manchester United

June 13th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

Mshambuliaji Odion Ighalo amesema kikosi cha sasa cha Manchester United kipo katika hali nzuri tayari kwa msimu wa ligi ya EPL kikisubiri kwa hamu mechi hizo kurejelewa.

Michuano ya ligi hiyo Kuu ya Uingereza (EPL) zitarejelewa katikati mwa juma lijalo ambapo United wataanza na Tottenham Hotspur Ijumaa, katika mechi ambayo Ighalo anatarajia timu yake kung’ara.

Ighalo ambaye mkataba wake ulitarajiwa kumalizika mwaka huu alikubali mkataba mpya ambao utamalizika Januari 2021.

Raia huyo wa Nigeria alikuwa katika timu iliyotoka sare 4-4 kwenye mechi ya kupimana nguvu miongoni mwa wachezaji wa United, Jumanne ambapo aliifungia timu yake mabao mawili.

“Nitaendelea kuweka bidii mazoezini, huku nikilenga kuvuma zaidi katika mechi za usoni,” aliwaambia waandishi kupitia kwa mtandao rasmi wa klabu hiyo ya Old Trafford.

“Nimeimarika kwa kiasi kikubwa baada ya kufanya mazoezi makali ya wiki mbili. Najisikia kuwa katika hali nzuri ya kung’ara mechini iwapo nitapewa nafasi kikosini. Nangojea kwa hamu mechi ya Ijumaa dhidi ya Spurs.”