Michezo

EPL ina kasi ya kipekee – Naby Keita

February 28th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

KIUNGO wa Liverpool Naby Keita amefunguka na kukiri kwamba Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ina kasi na hadhi kuliko Ligi ya Ujerumani (Bundesliga) na anaendelea kuzoea mtindo wa mchezo nchini Uingereza akilenga kung’aa.

Keita,24 alimwaga wino kwenye kandarasi ya kudumu ugani Anfield mwishoni mwa msimu 2017/18 na amekuwa akionyesha mchezo duni kila mara anapowajibishwa na mkufunzi wa Liverpool Jurgen Klopp.

Raia huyo wa Guinea aliyetambulika sana akisakatia RB Leipzig kwa uwezo wake wa kubuni nafasi za kufunga mabao ameweza kubuni nafasi moja tu ya kufunga katika mechi 24 alizoshiriki kwenye mashindano mbalimbali kwenye Ligi ya Uingereza.

Hali hiyo ni kinyume na msimu miwili akisakatia RB Leipzig ambapo alifunga mabao 16 na kusaidia kuzalisha mabao mara 14 huku akiafikia ufanisi wa juu msimu wake wa kwanza Ujerumani kwa kutajwa katika timu bora ya Bundesliga msimu wa 2016/17.

“Mpira ya hapa huchezwa kwa kasi sana kuliko Ujerumani. Kwa sasa nipo sawa na naendelea kujifunza jinsi ligi hii imekuwa ikisakatwa. Hakuna kilicho rahisi katika soka,” akatanguliza

“Ni ukweli usiopingika kwamba nilivuma sana enzi zangu Ujerumani lakini nimekuja kwa timu kubwa ambayo kila mtu anawania kupangwa kwenye kikosi cha kwanza. Ni juu yangu kutia bidii ili kumdhihirishia kocha kwamba naweza kutamba,” akaendelea.

Hata hivyo kuimarika kwake katika mechi zilizopita kumeshuhudia kocha Jurgen Klopp akimsifia kwa kusema yeye ni mchezaji mzuri anayeweza kuifikisha timu hiyo mbali.

Keita ambaye alilishwa benchi kwenye mtanange kati ya Liverpool na Manchester United Jumapili Februari 24 aliingizwa katika dakika ya 87 kuchukua nafasi ya Georginio Wijnaldum kwenye ushindi wa 5-0 waliousajili Liverpool Jumatano Februari 27.

Mlinzi Virgil van Dijk na winga Sadio Mane walifunga mabao mawili kila moja straika mwenye asili ya Kenya Divock Origi pia akijipatia bao kwenye ushindi huo mkubwa.