Michezo

EPL: Liverpool kuagana rasmi na afisa mkuu mtendaji Peter Moore

July 31st, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

AFISA Mkuu Mtendaji wa Liverpool, Peter Moore anatazamiwa kuondoka rasmi uwanjani Anfield mwishoni mwa Agosti 2020 baada ya kuhudumu katika wadhifa huo kwa kipindi cha miaka mitatu.

Nafasi ya Moore itatwaliwa sasa na Billy Hogan ambaye kwa sasa ni mkurugenzi msimamizi na afisa mkuu wa masuala ya kibiashara kambini mwa Liverpool.

Kwa miaka mitatu iliyopita, More ameshuhudia Liverpool wakirejea katika ubora wao wa zamani kiasi cha kujinyanyulia ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya miaka 30 ya kusubiri, ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Kombe la Dunia la FIFA.

“Haya ni mafanikio makubwa ambao tumeongozwa na kocha Jurgen Klopp, wachezaji na maafisa wetu wote katika benchi la kiufundi kupata. Kikosi cha Liverpool kimerejesha hadhi yake ya zamani na kwa sasa ni tishio kubwa kwa mpizani yeyote barani Ulaya na duniani,” akasema Moore.

“Hizi ni kumbukumbu zitakazodumu kwangu milele. Kwa kweli tulistahiki kutamba jinsi tulivyofanya baada ya kufanya yote tuliyoyafanya!” akaongeza kinara huyo.

Hadi kutua kwake kambini mwa Liverpool, Moore ambaye atarejea kwao Amerika, aliwahi kuwa mfanyakazi wa masuala ya teknolojia katika kampuni za Sega, Microsoft, EA Sports na Reebok ambayo hutengeneza vifaa vya michezo.

“Nilikuja Liverpool mnamo 2017 baada ya kuhudumu Amerika kwa zaidi ya miaka 30. Nimekuwa na kipindi spesheli sana uwanjani Anfield,” akasema Moore.