Habari za Kitaifa

EPRA yafunga vituo 18 kwa kuuza mafuta yaliyoghushiwa

January 6th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MAMLAKA ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA) imefunga vituo 18 vya kuuzia mafuta kwa madai ya kuuza mafuta yaliyoghushiwa.

Kwenye taarifa, Jumamosi, mamlaka hiyo ilisema kuwa kati ya Oktoba na Desemba 2023, ilifanya uchunguzi kuhusu bidhaa za mafuta zinazouzwa katika sehemu tofauti nchini.

Kwenye matokeo ya uchunguzi wake, ilibaini kuwa baadhi ya vituo vilikuwa vikiuzwa petroli iliyoharibiwa au ambayo haikuwa imefikisha viwango vinavyotakikana.

“Tulifanya tafiti 7, 114 katika maeneo 1600. Kutokana na tafiti hizo, tulibaini kuwa maeneo 1,574 (asilimia 98.3) yalikuwa yakiuza mafuta yaliyofikisha viwango vilivyoruhusiwa. Hata hivyo, maeno 26 (asilimia 1.62) yalipatikana kutouza petroli iliyofikisha viwango vinavyohitajika,”
ikasema EPRA.

Kati ya vituo 26 vilivyopatikana kutozingatia kanuni zilizowekwa, vitano vilipigwa faini na kuruhusiwa kuendelea na shughuli zake baada ya kulipa faini hizo.

Matrela ya vituo viwili yalinaswa, baada ya kubainika yalikuwa yamebeba mafuta yaliyopangiwa kuuzwa katika mataifa ya nje.

Mafuta ya kituo kimoja yalinaswa, huku eneo la kuuzia mafuta hayo likiharibiwa kwa kuuza mafuta taa yaliyokusudiwa kuuzwa katika mataifa ya nje.

Vituo vingine 18 vilifungwa.

Vituo vilivyofungwa vimo katika kaunti za Tharaka Nithi, Bungoma, Homa Bay, Embu, Kajiado, Busia, Kakamega, Kirinyaga, Taita Taveta, Nandi, Nakuru, Laikipia, Baringo na Siaya.