Habari za Kitaifa

Epra yajitenga na mlipuko wa Embakasi

February 4th, 2024 1 min read

NA BARNABAS BII

MAMLAKA ya Kudhibiti Kawi na Petroli (Epra) imejitenga na lawama kuhusu mlipuko wa gesi eneo la Embakasi ulioua watu watatu na kujeruhi zaidi ya 200.

Mkurugenzi Mkuu wa Epra, Daniel Kiptoo, alisema mmiliki alinyimwa leseni ila akaendelea kufanya kazi kinyume cha sheria.

“Tulibomoa eneo hilo haramu mara tatu na hata kumyima leseni,” alisema Bw Kiptoo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha NTV.

Bw Kiptoo alisema ingawa kampuni hiyo ilikuwa na leseni ya kusafirisha LGP, ilikuwa ikijaza gesi kutoka kwa lori katika kituo hicho kisicho halali na kusababisha mlipuko huo.

“Tuna kikosi cha uangalizi na utetezi kufuatilia miundo kama hii haramu lakini pia tunawarai Wakenya kuwa macho na kuripoti utendakazi kama huo kwa mamlaka husika,” akaomba Bw Kiptoo.

Alisema mamlaka hiyo inashirikiana na vyombo vingine vya usalama na maafisa wa mashtaka ili kuwachukulia hatua watu wanaokiuka kanuni za nishati na mafuta.

“Tunashirikiana na idara mbalimbali na tutawachukulia hatua wahusika,” akaongeza Bw Kiptoo.