Michezo

Equity Bank yawika kwenye michezo ya mashirika ya kifedha

September 22nd, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Co-operative Bank ilijiongezea tumaini la kufuzu kushiriki robo fainali za kuwania taji la Mashirika ya Kifedha nchini (Interbanks) ilipochoma Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) magoli 5-1 kwenye mechi iliyochezewa uwanja wa Kenya School of Monetary Studies (KSMS) jijini Nairobi.

Nayo Equity Bank ilijikatia tiketi ya robo fainali ilipotwaa mabao 3-0 dhidi ya Credit Bank huku Kenya Banks Sacco iliumwa magoli 4-1 na National Bank of Kenya(NBK) uwanjani humo.

Co-operative ya kocha, Peter Mukenga ilianza mechi hiyo kwa kishindo huku Samuel Onyango akipiga ‘Hat trick’ ndani ya dakika 20. UoN ilionyesha dalili za kuzinduka dakika ya 25 pale Collins Mkauta alipoitingia bao lililogeuka kuwa la kufuta machozi.

Hata hivyo Co-operative iliongeza bao la tatu kupitia Joash Ochieng dakika tano kabla ya kipindi cha mapumziko. Kipindi cha pili, Welson Peino alitingia Co-operative bao la tano na kufikisha alama 13 baada ya kucheza mechi zote sita. ”Nashukuru wezangu kwa kuonyesha mchezo safi na kuzoa alama zote muhimu,” alisema Allan Odhiambo.

Wanasoka wa akiba wa Co-operative wakifuatilia wenzao walipocheza na Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) kuwania taji la Mashirika ya Kifedha nchini (Interbanks) ugani KSMS, Nairobi. Co-opeartive ilishinda magoli 5-1. Picha/ John Kimwere

Mabingwa Equity Bank ilitandaza soka safi na kufanya wapinzani wao kukosa maarifa. Mfungaji hodari, Derrick Ayisi, Abushir Abubakar na Brian Kipkemboi kila mmoja aliitingia bao moja na kuvuna pointi zote muhimu.

Naye Byronne Otieno alipiga kombora mbili safi, huku Marvin Agumba na Ben Okello kila mmoja akicheka na wavu mara moja na kusaida NBK kufanya kweli. Bao la Kenya Bankers Sacco lilifunikwa kimiani na Calvin Oruya.

Katika voliboli ya wanawake, Barclays of Kenya (BBK) na KCB kila moja ilisajili pointi tisa na kutwaa uongozi wa mapema kwenye mechi hizo zinazochezwa kwa mtindo wa ligi. Nazo Co-operative Bank, Central Bank of Kenya (CBK), Equity Bank kila moja iliandikisha alama sita.

Wachezaji wa Standard Chartered kabla ya kukabili Commercial Bank of Africa(CBA) katika voliboli ya wanaume kuwania taji la Mashirika ya Kifedha nchini (Interbanks) ugani KSMS, Nairobi. Standard Chartered ilishinda seti 3-0. Picha/ John Kimwere

KCB iliandikisha ushindi wa mechi mbili kwa seti 3-0 kila moja mbele ya Stanbic Bank na I & M kabla ya kuzaba Equity Bank seti 3-1. Warembo wa BBK waliteremsha mchezo safi na kukomoa Commercial Bank of Africa(CBA), Co-operative Bank na National Bank of Africa (NBA) kila moja seti 3-0.

Licha ya Equity Bank kuyeyusha mechi moja ilifanikiwa kuvuna alama sita muhimu baada ya kuzoa seti 3-0 mara mbili dhidi ya Stanbic Bank na Standard Chartered. Nayo Co-operative ilinyuka CBA na CBK seti 3-0 kila moja huku CBK ikisajili ufanisi wa mechi mbili seti 3-0 kila moja mbele ya CBA na NBK.

Kwenye ya mchezo huo kwa wanaume, Co-operative iliandikisha alama 12 baada ya kushinda mechi nne kwa seti 3-0 kila moja dhidi ya Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN), Postbank, BBK na CBA.