Habari Mseto

Equity kufadhili masomo ya wanafunzi 12 wa Trans Nzoia

January 2nd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WANAFUNZI 12 kutoka kaunti ya Trans Nzoia wamefaidi na msaada wa masomo unaotolewa na Benki ya Equity.

Akiwatangaza walioteuliwa kufaidi na ruzuku hiyo ya masomo, meneja wa benki hiyo tawi la Kitale , Bw Michael Chege alisema wanafunzi hao wanatoka familia maskini.

Bw Chege alisema kulikuwa na maombi 600 na miongoni mwao watoto 100 walitoka jamii zilizozamishwa kabisa na hali ya uchochole na umaskini.

Meneja huyo wa Benki alisema ilibidi tu wawateue wanafunzi 12 waliotakiwa kutoka kaunti hiyo na kuwaacha wale wengine ambao pia Wanakandamizwa na umaskini.

Mwaka uliopita wanafunzi 25 waliteuliwa kutoka kaunti hiyo.

Bw Mwangi alitoa wito kwa serikali ya kaunti ya Trans-Nzoia iwape basari wanafunzi ambao hawakubahatika kuorodheshwa katika mpango huo wa Benki ya Equity.

Meneja huyo alisema wanafunzi walioteuliwa hapo awali wamekuwa msaada mkubwa kwa familia zao kwa vile baadhi yao wamewajengea wazazi wao nyumba.

Alisema wanafunzi walioteuliwa na kuhitimu sasa ni mabalozi wema katika jamii.

Walioteuliwa watajiunga na wanafunzi wengine 1,000 katika sherehe itakayofanyika chuo kikuu cha Kenyatta Januari 4, 2019