Habari Mseto

Equity na kaunti ya Murang'a wajadili ushirika wa Sh5 bilioni kufadhili huduma za afya

August 15th, 2020 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

BENKI ya Equity na Serikali ya Murang’a zinajadiliana kuhusu ushirika wa kitita cha Sh5 bilioni kufadhili miradi ya afya katika kaunti hiyo.

Kwa mujibu wa Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria, ushirika huo unalenga kuzindua hospitali kadha spesheli katika eneo hilo ambapo wenyeji watakuwa wakipokezwa huduma kwa malipo ya chini na kwingine, bila malipo pale inawezekana.

“Tunalenga kuzindua hospitali spesheli ya kushughulikia magonjwa ya meno na macho katika kaunti ndogo ya Maragua; ya kutibu magonjwa ya mifupa; nyingine ya kushughulikia magonjwa ya watoto; tuzindue nyingine ya kushughulikia waathiriwa wa saratani na pia nyingine ya kusaidia walio na shida za kupumua,” akasema.

Alisema kilele cha miradi hiyo ni kujengwa kwa hospitali ya ukufunzi ya kiwango cha Level Six na ambapo tayari kaunti imehifadhi kipande cha ardhi ukubwa wa ekari 10 kufanikisha ujenzi huo karibu na mji wa Thika.

Alisema analenga miradi hiyo iwe imekamilika na iwe ikitoa huduma kwa wenyeji kabla ya 2022 ambapo atastaafu kama gavana ambapo atakuwa amehudumu kwa kipindi cha miaka 10 na ambapo Katiba imemzima kuwania tena.

Wa Iria alifichua kuwa tayari Equity imekubali kuwa ndani ya Wakfu wa kufanikisha miradi hiyo.

Mkurugenzi wa Equity Dkt James Mwangi aliambia Taifa Leo kwamba “sihitaji kushinikizwa kujiunga na mpango wa manufaa kama huu kumaanisha niko tayari.”

Alisema Kaunti ya Murang’a daima itabakia kuwa kiungo muhimu cha benki ya Equity kwa kuwa “hapa ndipo tulianza huduma zetu tukiwa Equity Housing Finance na ambapo wakulima wa majanichai na wale wa kahawa ndio walikuwa mtaji wetu asili.”

Akasema: “Utuonavyo sasa, watu wa Murang’a ndio walitupa msingi wetu thabiti na sote tunajua kuwa kaunti hii ndiyo kitovu cha Benki ya Equity na kujiunga nao katika hali za maendeleo ni furaha yetu.”

Dkt Mwangi alisema kuwa pendekezo hilo la ushirika litawasilishwa katika bodi ya usimamizi ya Equity na ambapo “matumaini ni kwamba tutakuwa na jibu la kuwapa watu wa Murang’a kila sababu ya kutabasamu.”

Aliongeza kuwa Benki ya Equity imezindua kitengo cha afya na ambacho malengo yake ni kusaidia taifa hili kuafikia huduma bora za kiafya.