Equity yakana kumpa Aydin mkopo wa Sh15 bilioni

Equity yakana kumpa Aydin mkopo wa Sh15 bilioni

Na CHARLES WASONGA

BENKI ya Equity imekana madai ya Naibu Rais William Ruto kwamba ilimpa mkopo wa Sh15 bilioni mwandani wake, Mturuki Harun Aydin.

Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo Gerald Warui, Jumatano aliwaambia wabunge kuwa benki hiyo haijawahi kupokea simu kutoka kwa Dkt Ruto ambaye alidai kumsaidia mgeni huyo aliyefurushwa nchini mapema Agosti.

“Hatuna mteja au ushirikiano wa kibiashara na mtu kwa jina Harun Aydin. Vilevile, benki ya Equity haijampa mkopo wa aina yoyote,” Bw Warui akaeleza alipofika mbele ya wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha na Mipango, Nairobi.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mwakilishi wa Wanawake Homa Bay, Gladys Wanga ambayo inachunguza madai ya Dkt Ruto kwamba alimsaidia Aydin kupata mkopo wa Sh15 bilioni kufadhili ujenzi wa kiwanda cha kujenga chanjo ya Covid-19 nchini Uganda.

Kamati hiyo ilianzisha uchunguzi huo kufuatia madai ya Naibu Rais kwamba, kwa kupiga simu, alimsadia Aydin, aliyedai kuwa mwekezaji, kupata mkopo wa Sh15 bilioni kufadhili mradi huo.

“Nilipokuwa Uganda mwezi jana, Rais Museveni alikuwa amenialika nizindue ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza chanjo dhidi ya corona. Nilialikwa kwa sababu mwekezaji alikuja hapa afisini mwangu miaka miwili iliyopita na kuniomba nimuunganishe na benki ya Equity ili aweze kupata mkopo. Nilinyanyua simu na kupigia benki hiyo kuiomba imsaidie mwekezaji huyu kutoka Afrika Mashariki. Mwekezaji huyo alifaulu kupata mkopo wa Sh15 bilioni na akaenda Uganda kuanzisha kiwanda hicho,” Dkt Ruto akasema kwenye mahojiano katika runinga ya Inooro.

Alitoa madai hayo siku mbili baada ya Bw Aydin kufurushwa kutoka nchini mnamo Agosti 9, siku tatu baada ya kuwasili nchini kutoka Uganda.

Mturuki huyo ni miongoni mwa wandani wa Dkt Ruto ambao walipangiwa kusafiri naye hadi Uganda mnamo Agosti 2, lakini Naibu Rais akazuiliwa kusafiri kwa misingi kuwa hakupata idhini kutoka Ikulu.

Hata hivyo, Bw Aydin na wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Benjamin Tayari (Kinango) na Oscar Sudi (Nandi Hills) waliopangiwa kuandamana na Dkt Ruto katika ziara hiyo ambayo alidai ilikuwa ya “kibinafsi”.

Mturuki huyo alikamatwa na maafisa wa polisi katika uwanja wa ndege wa Wilson dakika chache baada ya kuwasili nchini mnamo Agosti 7, na kuzuiliwa korokoroni kwa tuhuma za kuhusika na ugaidi.

Hata hivyo, Dkt Ruto alimtetea vikali Bw Aydin akidai ni mwekezaji halali ambaye “anahangaishwa kutokana na sababu za kisiasa na uhusiano wake na mimi.”

You can share this post!

Kalonzo aondolewa doa la unyakuzi Yatta

ARTETA: Ana wiki sita tu!