Habari Mseto

ERC yaongeza bei ya mafuta tena

November 14th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Kuanzia Jumatano saa sita za usiku, waendeshaji wa magari na Wakenya kwa jumla watanunua mafuta kwa bei ya juu.

Hii ni baada ya Tume ya Kudhibiti Kawi (ERC) kutangaza kuongezwa kwa bei ya petroli, dizeli na mafuta taa kwa kati ya Sh2 na Sh4.

Tume hiyo Jumatano ilitangaza kuongezwa kwa bei ya mafuta kwa muda wa mwezi mmoja ujao kutokana na kuongezwa kwa bei ya mafuta katika soko la kimataifa.

Mafuta ya dizeli ndiyo yaliongezewa bei kwa kiwango cha juu zaidi ambapo Jijini Nairobi, kiwango hicho ni Sh3.11 kwa lita moja Jijini Nairobi.

Katika taarifa hiyo, tume hiyo ilisema mafuta aina ya Super Petrol yameongezwa kwa Sh2.38 Jijini Nairobi ilhali wananchi wanaoishi humo watanunua mafuta taa kwa Sh2.99 zaidi kwa lita moja.

“Ongezeko hilo limetokana na kuongezwa kwa bei ya mafuta katika soko la kimataifa kwa asilimia 4.02 kwa pipa moja la Super Petrol,” ilisema ERC katika taarifa, ambapo pipa hilo lilinunuliwa kwa Sh7,290 Septemba na kuongezeka hadi Sh7,580 Oktoba.

Bei ya dizeli iliongezeka kwa asilimia 5.84 na mafuta taa iliongezeka kwa asilimia 5.80, ilisema ERC katika taarifa hiyo.

Mjini Mombasa petroli itauzwa kwa Sh115.48 kwa lita, dizeli Sh110.21 na mafuta taa Sh109.20 ambapo Nairobi bei itakuwa ni Sh118.11 kwa petroli, Sh112.83 kwa dizeli na Sh111.83 kwa mafuta taa.