Bambika

Eric Omondi: Kakangu Fred hakuuawa, ilikuwa ajali ya kawaida

Na SINDA MATIKO July 3rd, 2024 1 min read

MCHEKESHAJI Eric Omondi amekanusha tetesi na madai kuwa mdogo wake mchekeshaji Fred Omondi aliuawa.

Kufuatia kifo chake Fred aliyezikwa wikendi iliyopita, kumezuka utata kwamba kuna mkono ulihusika kwenye kifo chake.

“Ndugu yangu alipofariki kulikuwa na pikipiki na lile basi palipotokea ajali ila hatukumpata mwendeshaji pikipiki kipindi ajali ilipotokea. Hiyo sasa ndio ikaleta utata sana, kukakuwa na maswali mengi sana. Ila juzi tumempata mwenye pikipiki kumbe naye pia aliaga kwenye ajali hiyo. Yeye anaitwa Mutiso na alizikwa Alhamisi (wiki iliyopita) kule kwao Machakos hata tulitumia familia elfu hamsini na nikazungumza na ndugu yake,” Eric ameweka wazi.

Mcheshi huyo aidha aliongeza kuwa:

“Ajali ilipotokea na wakawa wanakimbizwa hospitalini, kwa sababu Fred alikuwa ni celeb, ikawa rahisi kutambuliwa. Upande wa Mutiso alichukuliwa na watu wengine waliompeleka hospitalini pia, na ni kama aliibiwa simu maana mwili wake ulipofikishwa na waliomfikisha pale hospitalini wakatoweka. Kwa hiyo mwili wake ukasajiliwa kwa watu wasiotambulika. Familia yake ilichukua siku tatu kuja kumpata. Kwa hiyo ilikuwa ni ajali ya kawaida, hakukuwa na cha ziada,” ameongeza Omondi.

Eric anasema ataishi kumbukumbuka mdogo wake kwani ndiye aliyeanza kumwandikia ucheshi na hata kumpelekea kuwa maarufu.

“Nikianza komedi, ndugu yangu ndiye alianza kuniandikia vichekesho vyangu, watu hawajui vichekesho vyangu maarufu vinavyokumbukwa na wengi ni yeye ndiye aliyeniandikia. Kwa hiyo nitamuenzi kuwa mtu aliyenipa chanzo cha kuja kutoka na kuwa maarufu kupitia komedi.”

Fred Omondi aliaga baada ya boda boda aliyokuwa akisafiria kugongana na basii la dala dala. Mchekeshaji huyo alifariki papo hapo.