Bambika

Eric Omondi kufanya mazungumzo na Jackie Maribe kujiondolea lawama ya ‘deadbeat’

January 24th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MCHEKESHAJI Eric Omondi amebainisha wazi kuwa anataka kujiondolea lawama ya ‘deadbeat’, jina linalotumiwa kumrejelea mzazi ambaye amekwepa majukumu ya kulea mwanawe au wanawe.

Hii ni ishara ya Erico, kama anavyofahamika na wengi, kuthibitisha ni baba wa watoto wawili kutoka kwa wanawake wawili tofauti.

Katika mahojiano na kituo kimoja nchini, Erico alisema hataweza kujificha kuwa alifanikiwa kupata mtoto wa kiume na mwanahabari Jacque Maribe.

Kwa miezi kadhaa sasa kwenye mitandao ya kijamii, wengi wamekuwa wakizungumzia mtoto wake Erico na mke wake Lynne.

Erico sasa amesema kuna baadhi ya mambo ya hapo nyuma yalitokea ikiwemo kudai kwamba alitaka vipimo vya DNA na mtoto huyo wa mtangazaji huyo wa runinga.

Mchekeshaji huyo alisema hivi karibuni, atafanya mazungumzo na mwanahabari Jacque ili kupata njia ya kumlea mtoto wao.

“Yule ni damu yangu, ni mtoto wangu mvulana. Mimi nina watoto wawili, mvulana na msichana. Mwanangu na Jacque nitamfundisha, nitamlea, nitaishi na yeye kwa sababu ni mtoto wangu,” akasema Erico.

Mapema Januari, mke wake Lynne aliingia mitandaoni kujibu maswali kutoka kwa mashabiki.

Kuna waliomuuliza ikiwa anafahamu kuwa mumewe ana mtoto mwingine.

Lynne akijibu swali hilo, alidai kuwa yeye ndiye mwanamke wa kipekee aliye na mtoto na Erico.

Kwenye mahojiano, baba huyo wa watoto wawili, alimtetea Lynne na kusema kwamba ni mpenzi wake na chochote anachokisema anajiamini kwa maelezo yote.

Mnamo Juni 2023, Jacque alivunja kimya baada ya Erico kudai alikuwa amemzuia kufanya vipimo vya DNA kwa mtoto huyo.

Mrembo huyo wa runinga alitoa onyo kali kwa mchekeshaji huyo na kubainisha kuwa amechoshwa na uongo wake.

“Anadhani uzazi ni uchekeshaji. Anadanganya kuhusu kila kitu! Acha jina langu na mtoto wangu nje ya vichekesho vyako Eric! Nimechoka,” akasema Jacque.