Bambika

Esther Musila amuaibisha mwanamke tapeli aliyedai Guardian Angel ni mhanyaji

January 17th, 2024 1 min read

NA ELIZABETH NGIGI

ESTHER Musila, mke wa mwanamuziki wa nyimbo za Injili Guardian Angel, amefichua jinsi mwanamke tapeli alivyotaka kumtowanisha pesa, akidai alikuwa na ushahidi wa mumewe kuchovya asali nje ya ndoa.

Katika video kwa mitandao ya kijamii, Musila mwenye umri wa miaka 53 na mama wa watoto watatu alisimulia matukio hayo ya Januari 10, 2024.

Musila alifichua jinsi ambavyo mwanamke huyo afriti, ambaye inadaiwa ni wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na mmiliki wa kilabu kimojawapo, alimjia akiwa na kile alidai ni ushahidi wa tabia ya ‘uhanyaji’ ya Guardian Angel.

Mwanamke huyo alidai kuwa na ushahidi wa ujumbe wa malipo ya M-Pesa na ujumbe mfupi unaodaiwa kutumwa kati ya Guardian Angel na kimada.

Ujumbe wa mwanamke mchanganishaji ulisema: “Wewe ni mwanamke wa heshima zake, mnyenyekevu, mwenye akili timamu na mcha Mungu. Je, kwa siku za hivi karibuni huenda pengine umekuwa ukimshuku mumeo kuwa ana mpango wa kando? Hustahili haya.”

Mwanamke huyo mchonganishaji wa wapendanao alidai kwamba alikuwa na uwezo wa kujionea kamera za CCTV na pia alifanikiwa kupata risiti za malipo kupitia huduma ya M-Pesa.

“Huyu mwanamume akiendelea hivi atakuambukiza maradhi ya zinaa,” akaendelea mwanamke huyo akidai kimada aliyehusika alikuwa binti ya mwanasiasa.

Akamtaka Musila kujiwekea ‘ufichuzi’ huo kuwa siri.

Lakini Musila, alikataa kuingizwa boksi na mchonganishi huyo aliyetaka pesa.

“Kwa sasa nikiwa na umri wa miaka 53, siwezi nikamfuatilia mwanamume. Kile anataka kukifanya, acha afanye. Hakuna kile ninachoweza kuzuia.”

Baada ya ‘kibomu’ hicho Musila alifanya upelelezi wake, ambapo simu ya Guardian Angel ilinuswa ikagundulika kumbe ulikuwa ni uvunmi tu.