Habari

Ethiopia yaomboleza Waziri Mkuu akitoa hakikisho hali Amhara imedhibitiwa

June 25th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

ADDIS ABABA, ETHIOPIA

BENDERA nchini Ethiopia zilipeperushwa nusu mlingoti Jumatatu, serikali ilipotangaza siku moja ya maombolezi kufuatia mauaji ya maafisa wanne wa ngazi za juu mnamo Jumamosi.

Runinga zilipeperusha salamu za pole kutoka kwa viongozi wa maeneo na serikali kuu, viongozi wa kidini nao wakitoa wito wa amani.

Hali ya huduma za Intaneti kukatizwa jijini Addis Ababa iliendelea ingawa wakazi walionekana wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.

Serikali ilitangaza kuwa jaribio la kupindua serikali katika jimbo la Amhara lilitibuliwa, japo mkuu wa majeshi Seare Mekonnen aliuawa.

Jenerali Mekonnen pamoja na Meja Jenerali (Mstaafu) Gezai Abera waliuawa Jumamosi katika makazi ya mkuu huyo wa majeshi jijini Addis Ababa, na mlinzi wake.

Tukio hilo lilitokea saa chache baada ya jaribio la kupindua serikali jimbo la Amhara kutibuliwa, ingawa Rais wa jimbo hilo Ambachew Mekonnen na mshauri wake Ezzez Wassie waliuawa.

Kujeruhiwa

Mwanasheria Mkuu wa Amhara Migbaru Kebede, alijeruhiwa na anaendelea kupokea matibabu hospitalini.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed alilaani kitendo hicho, na kutangaza kuwa majeshi ya nchi hiyo yataendelea kuilinda.

“Hali katika jimbo la Amhara imedhibitiwa na sasa linasimamiwa na serikali kuu kwa ushirikiano na serikali ya eneo hilo,” ujumbe kutoka afisi ya Waziri Mkuu ulieleza.