Ethiopia yatangaza hatua dhidi ya TPLF

Ethiopia yatangaza hatua dhidi ya TPLF

Na AFP

SERIKALI ya Ethiopia imetangaza kuwa imekomboa miji miwili muhimu iliyokuwa imetwaliwa na wapiganaji wa kundi la waasi Tigray People’s Liberation Front (TPLF).

Kukombolewa kwa miji ya Dessie na Kombolcha, iliyoko eneo la Ahmhara, ni sehemu ya msururu wa ushindi ambao umeandikishwa na serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed siku za hivi majuzi dhidi ya TPLF.Miji hiyo ilitekwa mwishoni mwa Oktoba mwaka huu na kuibua hofu kwamba huenda waasi hao wakaelekea jiji kuu Addis Ababa.

“Miji ya Dessie na Kombolcha imekombolewa na muungano wa vikosi vyetu vya usalama,” Idara ya Mawasiliano ya Serikali ilisema Jumatatu jioni.Wiki iliyopita serikali ilitangaza kuwa wanajeshi wake walikomboa kituo cha UNESCO World Heritage kilichoko katika mjini wa Lalibela ambao ulitekwa na TPLF mnamo Agosti mwaka huu.

Kufanikiwa kwa serikali ya Abiy kukomboa maeneo mbalimbali kumetoa mwelekeo tofauti katika mapigano nchini Ethiopia ambayo yamedumu kwa miezi 13.Mwezi jana, Abiy alitangaza kuwa serikali yake iko tayari kwa vita baada ya TPLF kutwaa majimbo matatu.

Tangu waziri huyo mkuu alipotoa tangazo hilo, serikali ilisema kuwa imekomboa miji kadha midogo, ukiwemo mji wa Lalibela, maarufu kutokana na uwepo wa makanisa yaliyojengwa katika Karne ya 12.Lakini kwenye taarifa Jumapili, kiongozi wa kundi la TPLF, Debretsion Gebremichael alikanusha madai kuwa serikali ya Ethiopia imekuwa ikiandikisha msururu wa ushindi.

Alisema wapiganaji wake bado wanajipanga katika maeneo mbalimbali na kamwe hawajalemewa kwa namna yoyote.Serikali ya Ethipia ilichukua msimamo mkali zaidi mnamo Oktoba TPLF walipokaribia Addis Ababa na kuzua hofu wangepindua serikali.

Tangu wakati huo, fununu kwamba waasi hao wanaelekea kuteka jiji hilo kuu zilichangia mataifa ya kigeni kama vile Amerika, Ufaransa na Uingereza kushauri raia wao kuondoka Ethiopia “haraka iwezekanavyo”.Serikali imepuuzilia mbali uvumi huo ulionezwa na viongozi wa TPLF ikisisitiza kuwa jiji la Addis Ababa, lenye zaidi ya watu milioni tano, ni salama.

Vita vilizuka pale, Abiy ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Nobel ya 2019, alituma wanajeshi katika eneo la Tigray kwa lengo la kukomoa uongozi wa TPLF.Alisema hatua hiyo ilitokana na hatua ya wapiganaji wa kundi hilo la waasi kushambulia kambi za jeshi la kitaifa katika zilizoko eneo hilo la kaskazini mashariki mwa Ethiopia.

Abiy alitangaza ushindi wa haraka wa majeshi ya serikali yake.Lakini waasi hao walijibu kwa mashambulio makali, na wakadhibiti eneo lote la Tigray kufikia Juni mwaka huu. Aidha, waliteka mji mkuu eneo hilo, Mekele, kabla ya kusonga hadi maeneo ya Amhara na Afar.

Maelfu ya watu waliuawa katika mapigano hayo, zaidi ya watu milioni mbili wakatoroka makwao na maelefu ya wengine wakasalia kuathiriwa na baa la njaa, kulingana na ripoti za Umoja wa Mataifa (UN).Aidha, kumeibuka ripoti za mauaji ya halaiki na vitendo vya ubakaji vilivyotekelezwa na wapiganaji kutoka pande mbili hasimu.

Kufikia sasa juhudi zinazoongozwa na Umoja wa Afrika (AU) za kukomesha mapigano hazijazaa matunda.Mnamo Jumatatu, Amerika na mataifa washirika wake yalielezea kukerwa na ripoti kwamba serikali ya Ethiopia imezuilia idadi kubwa ya raia kinyume cha sheria na kwa misingi ya kikabila.

You can share this post!

Klabu 12 kunogesha Jamhuri Cup Mombasa

Polisi aua 7 akiwemo mkewe kabla kujiua

T L