Makala

Eugene Wamalwa: Ruto anarejesha nchi kwa utawala wa Nyayo

January 7th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

ALIYEKUWA Waziri wa Ulinzi, Eugene Wamalwa amemsuta Rais William Ruto akidai “anarejesha nchi kwa utawala wa kidikteta”.

Kulingana na mwanachama huyu wa muungano wa upinzani, Azimio la Umoja, utawala wa Dkt Ruto hauna tofauti na ule wa Rais mstaafu Marehemu Daniel Arap Moi.

Kwenye video, kiongozi huyo wa chama cha DAP-K anaskika akisema utawala wa Rais Ruto ni sawa na wa Nyayo.

Nyayo ni jina la lakabu alilopewa Mzee Moi wakati akiwa mamlakani, na alipohutubia umma hakukosa kulitamka.

“Tusipofanya jambo kumzuia, ataturejesha enzi za Nyayo; utawala uliosheheni udikteta, na utaathiri uhuru wetu wa demokrasia kama nchi,” Bw Wamalwa akasema.

Akiapa kushawishi wafuasi wa upinzani kukaidi mapendekezo ya serikali ya Kenya Kwanza yanayokandamiza taifa, alisema Azimio haitakubali Kenya kurejeshwa kwa enzi za udikteta.

Waziri huyo wa zamani wa Masuala ya Haki, alisema matamshi ya Rais Ruto kwa Idara ya Mahakama ni ishara ya utawala wa kimababvu na kidikteta kufufuliwa.

Kiongozi wa nchi amenukuliwa akisema hatakubali Mahakama kutekwa nyara na mafisadi wanaokataa Wakenya kupata maendeleo.

Rais Ruto alitoa kauli hiyo, akionekana kukerwa na maamuzi ya Mahakama Kuu mwishoni mwa 2023 kusitisha utelezwaji wa Mpango wa Nyumba za Bei.

Mahakama ya Rufaa, hata hivyo, ilimpa Ruto nafuu ikiruhusu makato ya asilimia 3 ya pesa kwa wafanyakazi huku uamuzi wa rufaa ukisibiriwa kuamliwa mnamo Januari 10, 2024.

Mfanyakazi anakatwa asilimia 1.5 ya mshahara wake naye mwajiri kiwango sawa na hicho kwa minajili ya mpango huo.

Dkt Ruto anasema mradi huo unatishiwa na maajenti wa ufisadi, anaodai wameteka nyara Idara ya Mahakama.

“Tuombee taifa letu lisirejeshwe katika utawala wa kidikteta. Tumemsikia Mheshimiwa William Ruto akisema tunashuhudia ukandamizaji wa mahakama, na kama Waziri wa Mwisho wa Masuala ya Haki tunayoona leo hii si ukandamizaji wa mahakama ila ni mkandamizaji na dikteta anayeitwa William Ruto,” Bw Wamalwa akasema.

Wamalwa, katika serikali ya Rais mstaafu Marehemu Mwai Kibaki alihudumu kama Waziri wa Masuala ya Haki.

Dkt Ruto aidha anatetea mradi wa Nyumba za Bei Nafuu akisema umebuni zaidi ya nafasi 120, 000 za ajira huku ukilenga ujenzi wa nyumba 258,874 kila mwaka.

Kando na mradi huo, Eugene Wamalwa analalamikia kupitishwa kwa Sheria ya Fedha 2023 ambayo ilipendekeza nyongeza ya ushuru (VAT) wa mafuta kutoka asilimia 8 hadi 16.

Hatua hiyo imesababisha mfumko wa bei ya bidhaa muhimu za kimsingi.