Michezo

EUROPA LEAGUE: Sevilla yanyamazisha Manchester United

August 17th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MATUMAINI ya Manchester United kunyanyua ubingwa wa Europa League kwa mara ya pili chini ya kipindi cha miaka minne yalizimwa na Sevilla mnamo Agosti 16, 2020.

Hii ni baada ya miamba hao wa soka ya Uingereza kupokezwa kichapo cha 2-1 kwenye nusu-fainali iliyowakutanisha mjini Dusseldorf, Ujerumani.

Sevilla ambao ni mabingwa mara tano wa Europa League, walitoka nyuma na kusajili ushindi ambao uliwakatia tiketi ya kunogesha fainali itakayowakutanisha na mshindi nusu-fainali nyingine kati ya Inter Milan ya Italia na Shakhtar Donetsk ya Ukraine.

Nusu-fainali hiyo ya pili, ambayo pia itakuwa ya mkondo mmoja pekee, itachezewa nchini Ujerumani mnamo Agosti 17, 2020, siku nne kabla ya fainali kutandazwa Ijumaa ya Agosti 21.

Kiungo mzawa wa Ureno, Bruno Fernandes aliwaweka Man-United kifua mbele kupitia penalti ya dakika ya tisa. Ni bao lililowapa ari zaidi huku wakionekana kuwazidi wapizani wao maarifa katika takriban kila idara.

Ingawa hivyo, Sevilla wananolewa na kocha Julen Lopetegui, walisalia imara huku kipa wao Yassine Bounou akifanya kazi ya ziada na kupangua makombora makali aliyoelekezewa na mfumaji Marcus Rashford aliyeshirikiana vilivyo na Fernandes na kiungo Paul Pogba.

Fowadi wa zamani wa Liverpool, Fernandez Saez ‘Suso’ Joaquin alisawazishia Sevilla katika dakika ya 26 baada ya kukamilisha krosi aliyopokezwa na Sergio Reguilon kwa ustadi mkubwa.

Luuk de Jong ambaye ni kiungo wa zamani wa Newcastle United, alikizamisha kabisa chombo cha Man-United baada ya kufungia Sevilla bao la pili na la ushindi katika dakika ya 78.

Bao hilo lilitokana na utepetevu wa mabeki wa Man-United walioshindwa kudhibiti vilivyo krosi iliyopigwa na nyota wa zamani wa Manchester City, Jesus Navas.

Sevilla walifuzu kwa nusu-fainali baada ya kuwabandua Wolves kwa 1-0 mnamo Agosti 11, 2020. Walifungiwa bao hilo na Lucas Ocampos.

Kwa upande wao, Man-United walitinga hatua ya nusu-fainali baada ya kuwapiga FC Copenhagen ya Denmark 1-0 kupitia penalti ya dakika za mwisho iliyofungwa na Fernandes.

Sevilla ambao kwa sasa wametinga hatua ya nusu-fainali ya Europa League mara saba, wanajivunia rekodi ya kunyanyua ufalme wa Europa League mara nyingi zaidi na wametawazwa mabingwa katika misimu yote mitatu ambayo imewashuhudia wakifika awamu ya robo-fainali.