Makala

EVANS ONYANGO: Bidii na nidhamu ni muhimu katika usanii

February 2nd, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

NI kijana anayezidi kujituma kiume katika muziki wa injili kwa mtindo wa kizazi kipya anayepania kuibuka kati ya wasanii watajika miaka ijayo hapa nchini na duniani kwa jumla.

Ingawa bado muziki wake haujapata mashiko, anajivunia kunasa tuzo mbili kutokana na tambo zake.

Chipukizi huyu ambaye pia ametunukiwa kipaji cha wafawidhi (MC), anasema changamoto za kifedha kugharamia ada ya kurekodi video nzuri imefanya wengi wao kutopiga hatua kimuziki.

Evans Onyango Aliwa maarufu kama Mswaleh Mswazi anasema mbali na hayo bado hajavunjika moyo katika kazi ya muziki. Chipukizi huyu hutunga nyimbo zake kwa mtindo wa Afro-Bongo; mchanganyiko wa mdundo wa kiafrika na Bongo.

”Ninapania mengi katika jukwaa la muziki wa burudani maana ninaamini mazuri yapo njiani,” anasema na kuongeza kuwa ingawa miaka inazidi kuyoyoma, anagojea wakati wa Mungu maana utakapotimia tu kamwe hakuna atakayezuia.

Anadokeza kuwa kando na kutinga hadhi ya kimataifa katika muziki pia anataka kuanzisha brandi yake ili kukuza wanamuziki chipukizi nchini.

Kando na muziki tangu mwaka 2015 hufanya kazi kama MC na kampuni ya Treasure Communication Limited inayomilikiwa na Francis Mworia.

Mswaleh aliyeanza kujituma kwenye masuala ya muziki mwaka 2014, amefaulu kughani zaidi ya nyimbo 100 lakini amerekodi tambo tano pekee.

Mwishoni mwa mwaka uliyopita aliachia nyimbo inayokwenda kwa jina ‘Moto’ aliyowashirikisha wanamuziki Nesphory (Kidis) na John Kamau (JDA).

Tungo zingine zake ni’Mwikulu,’ ‘Nena nami,’ ‘Hossana,’ na ‘Deka Deka.’ Picha/ John Kimwere

TUZO

Anajivunia nyimbo ya ‘Mwikulu’ kumpatia tuzo ya ‘Teeniz Fresh and New Bongo Song/Artist of the Year 2015 zilizoandaliwa na Xtreem Teeniz Awards.

Kibao hicho kiliteuliwa kuwania tuzo kitengo hicho kwenye hafla ya makala ya kwanza mwaka 2014. Teke hiyo ilizoa tuzo hiyo licha ya kutofanya vizuri katika soka la muziki wa burudani.

Kadhalika alifanikiwa kutwaa tuzo ya msaniii bora wa kiume wa mwaka kupitia kibao cha ‘Deka deka’ kwenye hafla ya Migori County Music Awards 2017.

JOSE CHAMELEON

Anasema analenga kufikia kiwango cha kati ya wasanii wanaoendelea kupiga hatua katika ulingo wa muziki nchini kama Sauti Sol na Nyashinski watunzi wa ‘Melanie,’ ‘Short & Sweet,’ na ‘Malaika’ ‘Nakupenda’ mtawalia.

Na Afrika analenga kufikia Wizkid na Jose Chameleon waliofanya kazi matata kama ‘Star boy,’ ‘Money’ na ‘Mama roda’ pia ‘Kipepeo’ mtawalia.

SIO MCHOYO

Msanii huyu alizaliwa eneo la Airport-Kisumu Ndogo ambapo mwanzo alisomea Shule ya Msingi ya Fumbini Kaunti ya Kilifi kisha kumalizia elimu ya kiwango hicho kwenye Shule ya Ushindi Education Center-jijini Nairobi.

Chipukizi huyu sio mchoyo wa mawaidha anawaambia wenzake kuwa kamwe wasikate tamaa mbali wawe wavumilivu kwani bidii yao ndiyo itawawezesha kupiga hatua katika muziki wao miaka ijayo.

Kadhalika anasema hakuna aliyezaliwa kama anafahamu talanta yake mbali bidii, nidhamu na kujituma ndizo hufanya wanadamu kutambua taaluma yake.