Bambika

Eve Mungai achapa kazi akifunika tetesi za penzi kuingia mdudu

January 4th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

‘YOUTUBER’ Mungai Eve anaendelea kufanya kazi yake kama kawaida licha ya kuwekewa presha aeleze mambo wazi kuhusu uvumi wa kuachana na mpenziwe Director Trevor.

Hii ni baada ya kila mmoja kufuta picha za mwezake kwenye akaunti zao za mitandao ya kijamii.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Eve amevunja kimya kwenye chapisho moja la matangazo baada ya watumiaji wa mitandao kufurika hapo wakimtaka kuelezea kilichojiri.

Kwenye chapisho hilo la kibiashara, mashabiki wake walipoteza umakini kwa tangazo hilo na badala yake kumtaka ajibu ikiwa kweli penzi limeingia mdudu.

Katika sehemu ya kuchangia, mmoja wa mashabiki alimtaka Eve kumjibu.

Eve hata hivyo akimjibu mmoja wa wachangiaji hao akimshauri aweke zingatio kwa tangazo la kibiashara na baadaye atazungumzia uvumi huo.

“Halafu sasa utupigie stori yako baada ya hili (tangazo,” alichangia M.T.U.G.E.N.

Naye Eve akawa mwepesi kumjibu.

“Kwanza tumakinike,” akajibu Eve huku akiahidi kuwa “nitazungumzia baadaye.”

Msukumo huo kutoka kwa mashabiki, ulimfanya mmoja wao ambaye ni Collin Malik, kuingilia kati na kumnusuru mwanamaudhui huyo. Alimpa moyo kwa kumshauri kupuuza matukio ya sasa.

Eve alikubaliana naye kwa kupachika emoji za kuonyesha asilimia 100.

“Huyu binti anazingatia kazi yake tu… mdudu kwenye maisha yako ya mahusiano asikusumbue,” alisema Collin Malik.

Eve na Trevor wamekuwa kwenye mahusiano kwa zaidi ya miaka mitano. Hivi juzi Trevor aliandika kwenye mitandao ya kijamii atakuwa na mtoto wa kiume kupitia njia ya adoption yaani kuasili.

Siku moja baada ya ujumbe huo kuenea kwenye mitandao ya kijamii, wawili hao waliacha kufuatana kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakihisi ujumbe huo uliashiria pengine Eve kasusia kumzalia.