Makala

EVELYN MUKIRI: Nitarejea kwa kishindo katika majukwaa ya uigizaji

June 24th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

ANAAMINI anacho kipaji cha kufanya vizuri katika tasnia ya uigizaji na kutwaa tuzo za kimataifa kama Oscars, Emmys na Grammys kati ya zingine.

Anasema kuwa amepania kujituma kiume ili kutimiza ndoto ya kuibuka kati ya waigizaji mahiri duniani na kuwapiku wasanii mahiri kama Viola Davis mzawa wa Marekani.

Pia anasema anatamani sana kufikia upeo wa mwigizaji wa Hollywood mzawa wa hapa Kenya, Lupita Nyong’o.

Evelyn Mukiri maarufu Shani ambaye hufanya kazi ya Uhandisi katika kampuni moja jijini Nairobi anaorodheshwa kati ya waigizaji chipukizi wanaokuja wakilenga kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo.

Binti huyo anasema alisomea uhandisi maana maisha hayakumwendea vizuri hasa kutimiza azma yake kwa kuzingatia tangu akiwa mdogo alitamani sana kuhitimu kuwa rubani.

”Nimepania kurejea kwa kishindo katika masuala ya uigizaji baada ya kukawia kwa muda sasa,” anasema na kuongeza kwamba alivutiwa na uigizaji alipotazama filamu iitwayo ‘Salt’ kazi yake mwigizaji wa kimataifa Angelina Jolie mzawa wa Marekani.

Aidha msanii huyo anajivunia kuigiza filamu nyingi tu ikiwamo ‘Wanted,’ ‘Maleficent,’ ‘Mr and Mrs Smith,’ ‘Original,’ na ‘Girl Interrupted.’

Kando na hayo anasema akiwa nyumbani anapenda sana kutazama filamu mbali mbali ili kujifahamisha mengi kuhusu tasnia hiyo.

MPANGO WA KANDO

Kisura huyu anajivunia kushiriki filamu iitwayo ‘Nyundo Utosini’ iliyopata mwanya kupeperushwa kupitia runinga tatu hapa nchini (KBC, Maisha Magic East na K24).’

Kadhalika anajivuni kushiriki filamu nyingine mapema mwaka huu inayofahamika kama ‘Mpango wa Kando,’ chini ya kampuni ya Vuma Productions.

Filamu hiyo ipo jikoni amekwimishwa na mkurupuko wa virusi hatari vya corona. ”Katika mpango mzima napenda filamu ya Nyundo Utosini maana ndiyo iliokuwa ya kwanza kwangu pia kupeperushwa kupitia runinga kadhaa hapa nchini,” akasema.

PATIENCE OZOKWOR

Kwa waigizaji wa humu nchini kipusa huyu anasema angependa kufanya kazi nao ‘Shish’ (Tahidi High)’ pia ‘Shosh’ (Mother in Law). Kwa waigizaji wa Afrika anasema kwamba atamani sana kujikuta katika jukwaa moja na waigizaji mahiri kama Patience Ozokwor ambaye hushiriki filamu za Kinigeria (Nollywood).

”Kusema kweli napenda uigizaji wake kawaida ni mpole na mcheshi ila katika uigizaji hasumbuki kutoa picha ya mtu mbaya,” akasema.

Patience Ozokwor anajivunia kuigiza filamu nyingi ikiwamo ‘Blood Sister,’ ‘Mothers in Law,’ ‘Chief Daddy,’ ‘Sisters on Fire,’ na ‘The Wedding Party 2,’ kati ya zingine.

MAWAIDHA

Msichana huyu anashauri wasanii wenzake wanaokuja wawe wavumilivu, wasife moyo pia wala wasitamani kupata umaarufu wa haraka.

”Ingawa sijapata mashiko katika tasnia ya filamu ninafahamu sekta hii ina changamoto nyingi tu ambapo ili kufanya vizuri lazima tuwe makini,” alisema na kuongeza kuwa ni vyema kujiheshimu nyakati.