Everton wapiga Arsenal breki kali katika EPL

Everton wapiga Arsenal breki kali katika EPL

NA MASHIRIKA

ARSENAL walipoteza fursa ya kufungua mwanya wa alama nane kati yao na mabingwa watetezi Manchester City kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kupigwa 1-0 na Everton ugani Goodison Park.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa kocha Sean Dyche kusimamia kambini mwa Everton tangu aaminiwe kuwa mrithi wa Frank Lampard aliyetimuliwa wiki jana baada West Ham United kuwatandika 2-0 jijini London.

Ingawa Arsenal wangali kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 50, watajipata kwenye presha zaidi iwapo Man-City wanaokamata nafasi ya pili kwa pointi 45 wataangusha Tottenham Hotspur ugenini mnamo Februari 3, 2023.

Everton ambao sasa wana alama 18 kutokana na mechi 21, walifunga bao lao kupitia kwa James Tarkowski katika dakika ya 60.

Tofauti na Arsenal ambao wamepoteza mechi mbili kati ya 20 na ya kwanza kutokana na 14 zilizopita, Everton walijitosa ugani wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kutoshinda mechi 10 mfululizo tangu watandike Crystal Palace 3-0 ugani Selhurst Park mnamo Oktoba 22, 2022.

Everton waliokuwa wamepoteza mechi nne mfululizo za EPL uwanjani Goodison Park hapo awali, wamefunga angalau bao moja katika kila mojawapo ya michuano minne iliyopita ya nyumbani.

Mechi ya Februari 4, 2023 ilikuwa fursa maridhawa kwao kulipiza kisasi dhidi ya Arsenal waliowapepeta 5-1 katika mchuano wa mwisho wa msimu jana ligini. Arsenal wameangushwa sasa katika mechi tatu zilizopita dhidi ya Everton ugani Goodison Park.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ruto ateua Mwathethe kusimamia KEFRI

KWPL: Ulinzi Starlets wapiga Vihiga Queens 3-2 uwanjani...

T L