Michezo

Everton wapiga Arsenal na kuendeleza masaibu ya kocha Mikel Arteta

December 20th, 2020 3 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta amesema Arsenal “wako katika vita vikali” na wachezaji wake “kwa sasa wanaumiza zaidi” baada ya kupokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Everton uwanjani Goodison Park mnamo Disemba 19, 2020.

Ilikuwa mara ya nane kwa Arsenal kushindwa kutokana na mechi 14 za hadi kufikia sasa katika kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Huku Everton wakihakikisha kwamba kocha Carlo Ancelotti anasherehekea vyema maadhimisho ya mwaka mmoja wa ukufunzi kambini mwao kwa kutinga nafasi ya pili jedwalini, Arsenal walizidisha masaibu ya Arteta ambaye kwa sasa yuko katika hatari ya kutimuliwa.

“Tunahitaji kujituma zaidi ili kushinda mechi. Haiwezekani kwa Arsenal kuwa mteremko wa kila mshindani katika EPL. Hata hivyo, vijana walijitahidi na itatulazimu kuanza kushinda mechi ili kupata msukumo wa kutuaminisha kufanya vyema,” akasema kocha huyo raia wa Uhispania ambaye pia amewahi kuchezea Everton na Arsenal.

Chini ya Ancelotti, Everton kwa sasa wamebwaga Chelsea, Leicester City na Arsenal chini ya kipindi cha siku saba.

Kikosi hicho kilijipata uongozini katika dakika ya 22 baada ya Rob Holding kujifunga kutokana na kombora la Dominic Calvert-Lewin lililomwacha hoi kipa Bernd Leno.

Hata hivyo, walisawazishiwa na Nicolas Pepe katika dakika ya 35 kupitia penalti baada ya Tom Davies kumchezea visivyo beki Ainsley Maitland-Niles.

Ingawa bao la Pepe lilitarajiwa kuamsha ari ya Arsenal ya kusajili ushindi, ni Everton ndio waliopata goli la pili kupitia Yerry Mina mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Arsenal waliimarika katika kipindi cha pili huku David Luiz akishuhudia fataki yake ikigonga mhimili wa goli la Everton ambao pia walipoteza nafasi nyingi za wazi.

Kichapo ambacho Arsenal walipokezwa kiliwateremsha hadi nafasi ya 15 jedwalini kwa alama 14 kutokana na mechi 14.

Mwaka mmoja umepita tangu kocha Ancelotti atue Merseyside kutoka Italia kurasimisha kuajiriwa kwake na Everton. Kabla ya kutia saini kandarasi aliyopokezwa, Ancelotti alihudhuria mchuano wa EPL uliowakutanisha Everton na Arsenal uwanjani Goodison Park. Mechi hiyo ilikamilika kwa sare tasa.

Kwa upande wake, Arteta aliyekuwa ameajiriwa na Arsenal siku chache kabla, alikuwa pia uwanjani na aliketi mbali kidogo na Ancelotti huku matarajio ya mashabiki yakiwa kwamba angeleta matumaini ya ufufuo mkubwa wa kikosi chao.

Mbali na Calvert-Lewin na Mina, wanasoka wengine walioridhisha zaidi kambini mwa Everton dhidi ya Arsenal mnamo Jumamosi ni sajili wapya wa Ancelotti – Abdoulaye Doucoure na Ben Godfrey.

Arsenal waliokosa huduma za fowadi na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang, waliponea chupuchupu kufungwa mabao mengi ya mapema huku Willian aliyetokea Chelsea mwishoni mwa msimu wa 2019-20, akishindwa tena kutamba ndani ya jezi za Arsenal.

Utovu wa nidhamu ambao umekuwa kitambulisho cha Arsenal katika mechi kadhaa zilizopita bado ulidhihirika baada ya Dani Ceballos kumchezea visivyo kiungo Mina. Hata hivyo, Ceballos aliponea sana kuonyeshwa kadi nyekundu.

Alama 14 zinazojivuniwa na Arsenal kufikia sasa ligini ni rekodi ya mwanzo mbaya zaidi wa msimu tangu 1974-75 ambapo walishinda mechi tatu pekee kutokana na mechi 14 za ufunguzi wa muhula.

Japo ushindi wa Kombe la FA mwishoni mwa msimu wa 2019-20 na wa Community Shield mwanzoni mwa muhula huu uliashiria ufufuo wa Arsenal chini ya Arteta, kikosi hicho sasa kimepiga jumla ya mechi saba za EPL bila ya kusajili ushindi wowote.

“Inakaribiana sana na hali nyinginezo ambazo zimekuwa zikitupata wiki chache zilizopita ambapo tulitamalaki mchuano, kumiliki asilimia kubwa ya mpira ila tukaishia kupoteza,” akatanguliza Arteta.

“Tulipata fursa kadhaa za kufunga. Lakini fataki za mwisho katika idara ya mbele na pasi ambazo viungo wavamizi wanafaa kuwapa washambuliaji wakamilishe hazipo kabisa. Tuna ulazima wa kuanza kushinda mechi kwa kuwa hilo ndilo jambo ambalo kwa sasa halifanyiki Arsenal,” akasema Arteta.

Everton kwa sasa wameshinda mechi mbili kati ya tatu zilizopita dhidi ya Arsenal ligini.

Baada ya kushinda mechi moja pekee kati ya saba za awali katika EPL, Everton kwa sasa wamejinyanyua na kushinda kila mojawapo ya mechi zao tatu zilizopita. Ni ufanisi ambao unawapa uhakika wa kusherehekea Krismasi wakiwa ndani ya mduara wa nne-bora kwenye msimamo wa jedwali kwa mara ya kwanza tangu 2004-05.

Arsenal hawajafunga bao lolote isipokuwa kupitia penalti kutokana na mechi tano zilizopita za EPL ugenini.

Holding anakuwa sasa sogora wa tatu wa Arsenal kujifunga katika EPL msimu huu baada ya Bukayo Saka dhidi ya Aston Villa na Aubameyang dhidi ya Burnley.

Pepe amehusika katika idadi kubwa zaidi ya mabao ambayo yamefungwa na Arsenal hadi kufikia sasa msimu huu. Nyota huyo raia wa Ivory Coast ndiye anaongoza orodha ya wafungaji bora wa Arsenal kwa mabao matano na amechangia mengine matatu.

Everton kwa sasa wanajiandaa kualika Manchester United kwenye robo-fainali za Carabao Cup mnamo Disemba 23 kabla ya kuwaendea Sheffield United kwa minajili ya mechi ya EPL mnamo Disemba 26 uwanjani Bramall Lane.

Kwa upande wao, Arsenal kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Manchester City kwenye robo-fainali za Carabao Cup kabla ya kualika Chelsea ugani Emirates kwa gozi la EPL.