Everton wasajili fowadi Andros Townsend na kipa Asmir Begovic

Everton wasajili fowadi Andros Townsend na kipa Asmir Begovic

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

EVERTON wamemsajili fowadi wa zamani wa Crystal Palace, Andros Townsend kwa mkataba wa miaka miwili na kujinasia pia huduma za kipa Asmir Begovic wa Bournemouth kwa kandarasi ya miezi 12.

Townsend, 30, alikuwa mchezaji huru tangu mkataba wake na Palace utamatike rasmi mnamo Juni 30, 2021. Anaungana sasa na kocha Rafael Benitez aliyewahi kumnoa katika kikosi cha Newcastle United.Kutua kwake ugani Goodison Park kunatarajiwa kupiga jeki safu ya mbele ya Everton ambao chini ya kocha mpya Benitez, wanajitahidi kujaza pengo la Theo Walcott aliyerejea Southampton mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Kusajiliwa kwa Begovic, 34, kutachochea viwango vya ushindani katika klabu ya Everton ambayo imekuwa ikijivunia maarifa ya kipa chaguo la kwanza katika timu ya taifa ya Uingereza, Jordan Pickford.Begovic ambaye pia amewahi kudakia Stoke City na Chelsea, anatarajiwa kuwa kizibo cha kipa Robin Olsen wa Uswidi aliyerejea AS Roma nchini Italia baada ya kipindi chake cha mkopo ugani Goodison Park kukamilika mwisho wa msimu wa 2020-21.

Townsend ambaye amechezea Uingereza mara 13, aliwahi pia kuwajibikia Tottenham Hotspur, Queens Park Rangers (QPR) na Newcastle United kabla ya kutua Palace mnamo 2016. Palace walimchezesha mara 36 na akafunga bao moja mnamo 2020-21 chini ya kocha Roy Hodgson ambaye sasa nafasi yake imetwaliwa na sogora wa zamani wa Arsenal aliyekuwa kocha wa Nice, Patrick Vieira.

Begovic aliingia katika sajili rasmi ya Bournemouth mnamo 2017 baada ya kuagana na Chelsea. Alikuwa amesalia na mwaka mmoja kwenye mkataba wake na Bournemouth ya Ligi ya Daraja ya Kwanza nchini Uingereza (Championship).

Aliwajibishwa na Bournemouth mara 51 mnamo 2020-21 na akasaidia kikosi hicho kutinga nusu-fainali za mchujo wa kufuzu kwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Walizidiwa maarifa na Brenford ambao sasa wanaendelea kujisuka upya kwa kampeni mpya za EPL mnamo 2021-22.

 

  • Tags

You can share this post!

Vipusa wa Joylove wanataka kurejea ligi ya daraja la kwanza

Celtic na Midtjylland nguvu sawa kwenye mchujo wa UEFA