Michezo

Everton yapigwa 2-0 na Southampton United beki Lucas Digne akionyeshwa kadi nyekundu

October 25th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

EVERTON walipokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Southampton katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Oktoba 25, 2020 uwanjani St Mary’s.

Ushindi huo uliosajiliwa na vijana wa kocha Ralph Hasenhuttl dhidi ya masogora wa mkufunzi Carlo Ancelotti ulipiga breki rekodi ya kutoshindwa kwa Everton ambao hadi walioshuka dimbani, walikuwa wamesakata mechi tano bila kupoteza.

James Ward-Prose aliwafungulia Southampton ukurasa wa mabao kunako dakika ya 27 kabla ya Che Adams kupachika la pili katika dakika ya 35. Fowadi Danny Ings alichangia magoli yote mawili ya Southampton.

Everton waliokuwa bila ya nahodha Seamus Coleman, walishuka dimbani wakiujivunia alama 13 kutokana na mechi tano za kwanza zilizowashuhudia wakiangusha Tottenham Hotspur, West Bromwich Albion, Crystal Palace na Brighton kabla ya kuambulia sare ya 2-2 dhidi ya Liverpool kwenye gozi kali la Merseyside mnamo Oktoba 17, 2020.

Gylfi Sigurdsson aliyevalia utepe wa unahodha kwa upande wa Everton dhidi ya Southampton alishuhudia makombora yake mawili yakigonga mwamba wa lango la Southampton huku akishindwa pia kumzidi maarifa kipa Alex McCarthy.

Beki Lucas Digne alionyeshwa kadi nyekundu katika mchuano huo baada ya kumchezea visivyo Kyle Walker-Peters. Ilikuwa mara ya pili mfululizo kwa mchezaji wa Everton kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya fowadi Richarlison Andrade pia kufurushwa uwanjani mwishoni mwa kipindi cha pili dhidi ya Liverpool mnamo Oktoba 17.

Mbali na kiu ya kuendeleza rekodi ya kuwa kikosi cha pekee ambacho hakikuwa kimepigwa katika EPL hadi kufikia jana, Everton walikuwa pia wakipania kusajili ushindi wa pili mfululizo dhidi ya Southampton ugenini kwa mara ya kwanza tangu Januari 1992.

Licha ya kichapo, Everton bado wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 13 sawa na Liverpool. Kwa upande wao, Southampton wanajivunia alama 10 sawa na limbukeni Leeds United na Crystal Palace waliosajili ushindi wa 3-0 na 2-1 dhidi ya Aston Villa na Fulham mtawalia.