Habari Mseto

Ezekiel Mutua afurahishwa na juhudi za Sakaja hamasisho kukabili Covid-19

April 28th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

AFISA Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Kukagua Filamu Nchini (KFCB) Ezekiel Mutua awatuza Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja na msanii Esther “Akothee” Akoth Sh50,000, kila mmoja, kwa kuendeleza uhamasisho kuhusu janga la Covid-19.

Hii ni baada ya Seneta Sakaja kuibua msisimko kwenye mitandao ya kijamii kwenye video iliyomwonyesha akiwaungana na wanawe wawili wakiimba wimbo wa “rap” unaoelimisha umma kuhusu njia za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Katika video hiyo, Sakaja na wanawe wa kiume, wanatumia ubunifu kuwasihi Wakenya kubadili mienendo na kuzingatia agizo la kutotangamana, kunawa mikono kwa sabuni na kutii kanuni za kafyu ili kushinda vita dhidi ya janga hili

Bw Mutua ametaja video hiyo kama “kazi nzuri ya ubunifu ya kutoa uhamasisho kuhusu Covid 19.

Aliongeza kuwa jumbe za Akothee kuhusu janga hilo zimekuwa za kuvutia mno

“Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja na wanawe ni washindi kwa kazi nzuri ya usanii ya kutoa uhamasisho kuhusu njia za kujikinga na Covid-19. Naye Esther Akoth, almaarufu Akothee anatwaa taji kama msanii aliyeimarika zaidi nchini Kenya. Katika siku za hivi karibuni jumbe zake mitandaoni zimekuwa za kuvutia zaidi. Wawili hao nawatuza Sh50,000!” Bw Mutua akasema kwenye ujumbe katika akaunti yake ya twitter.

Akothee, kupitia mtandao wa Instagram, amemshuru Bw Mutua kwa tuzo hiyo.

Na ametangaza kuwa atawasilisha pesa hizo kwa wanawake ambao hufanya kazi kwa vilabu vya usiku lakini wameachwa bila ajira kufuatia amri ya serikali ya kufunga biashara hiyo kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Wiki jana, msichana mwenye umri wa miaka 10, Salome Wairimu, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita, alisisimua Wakenya kutokana na wimbo wake “Janga la Korona” ambao umekopa midundo ya wimbo mmoja wa kizalendo.