Michezo

FA: Pep alivyopepetwa na Man U mpaka akakubali

May 27th, 2024 2 min read

LONDON, UINGEREZA

KOCHA Pep Guardiola anajilaumu kwa masaibu ya Manchester City kuvuliwa ubingwa wa Kombe la FA na Manchester United, akisisitiza kuwa ni mbinu zake uwanjani zilifeli wala sio kwa sababu walisherehekea kupindukia ushindi mara nne mfulilizo wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

City waliwasili ugani Wembley mnamo Jumamosi wakinusia historia ya kuwa timu ya kwanza kushinda mataji mawili katika msimu mmoja mara mbili mfululizo.

Hata hivyo, City waliduwazwa 2-1 na vijana wa kocha Erik ten Hag waliofurahia uongozi wa 2-0 wakati wa mapumziko kupitia mabao ya Alejandro Garnacho na Kobbie Mainoo.

City waliimarika katika kipindi cha pili baada ya Guardiola kutupa uwanjani Manuel Akanji na Jeremy Doku kujaza nafasi za Nathan Ake na Mateo Kovacic mtawalia na kusukuma beki John Stones kucheza katika safu ya kati, lakini bao la Doku dakika ya 87 halikutosha kuwezesha City kukamilisha ufufuo.

“Kongole kwa Man United. Nadhani mbinu zangu za mechi katika kipindi cha kwanza hazikuwa nzuri. Tuliimarika katika kipindi cha pili. Hata hivyo, kutokana na uamuzi wangu, hatukuwa katika nafasi nzuri za kuwashambulia. Hili lilikuwa kosa, mbinu zangu hazikuwa nzuri. Hazikufanya kazi,” akakiri Guardiola.

“Tunasikitika, lakini sherehe za kushinda ligi zitaendelea wiki hii,” akaongeza.

Washindi United walijizolea Sh330.1 milioni nao City wakaridhika na Sh165.0 milioni.

Ulikuwa ushindi mtamu kwa United waliomaliza ligi katika nafasi ya nane, kwani walifuzu Ligi ya Uropa kwa kusukuma Chelsea hadi Europa Conference League na Newcastle nje ya mashindano ya Bara Ulaya.

Pia, United, ambao walipoteza 2-1 dhidi ya City katika fainali ya Kombe la FA mwaka jana, walipiga breki rekodi ya Rodri kutoshindwa mechi 74 na kusitisha rekodi ya City kutoshindwa mechi 35.

Ten Hag, ambaye amekuwa na presha kali ya kufutwa kazi kwa sababu ya msimu mbovu, aliandikisha rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kuchapa City katika fainali ya kombe kubwa nchini Uingereza.

Ripoti zinadai kuwa kocha huyo Mholanzi atakutana na mmiliki Jim Ratcliffe na mkurugenzi wa michezo wa INEOS David Brailsford juma lijalo kutathmini msimu ulivyokuwa.

United walimaliza ligi katika nafasi ya nane, mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 30.

Hatima ya Ten Hag bado haijaamuliwa, ingawa inaaminika United tayari wana orodha ya makocha wanaoweza kuchukua mikoba yake ugani Old Trafford wakiwemo Thomas Tuchel na Kieran McKenna.