FA yashtumu tukio la ubaguzi wa rangi dhidi ya Saka, Sancho na Rashford

FA yashtumu tukio la ubaguzi wa rangi dhidi ya Saka, Sancho na Rashford

Na MASHIRIKA

SHIRIKISHO la Soka la Uingereza (FA) limeshtumu na kukashifu tukio la wanasoka Jadon Sancho, Marcus Rashford na Bukayo Saka kubaguliwa kirangi baada ya Three Lions kucharazwa na Italia kwenye fainali ya Euro mnamo Jumapili usiku jijini London.

Wachezaji hao watatu wa Uingereza walikosa penalti zao kwenye ushindi wa 3-2 uliosajiliwa na Italia baada ya kuambulia sare ya 1-1 kufikia mwisho wa muda wa ziada.

Kwa mujibu wa FA, maafisa wa usalama jijini London tayari wameanza uchunguzi kuhusiana na tukio hilo ambalo shirikisho limesisitiza kwamba “halitavumiliwa zaidi katika soka ya sasa.”

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, naye ameelezea mshangao wake baada ya tukio hilo na kushikilia kwamba Uingerez wanastahili kusifiwa kwa hatua kubwa iliyopigwa na kikosi cha kocha Gareth Southgate badala ya wanasoka wachache kulaumiwa kwa kichapo kutoka kwa Italia.

Wanasoka wote wa Uingereza wamekuwa akipiga goti kabla ya kipenga cha kuashiria kila mchuano kupulizwa kuashiria utayarifu wao wa kukabiliana vilivyo na matukio ya ubaguzi wa rangi.

Rashford aliwahi pia kubaguliwa kwa misingi ya rangi yake baada ya waajiri wake Manchester United kupoteza fainali ya Europa League dhidi ya Villarreal ya Uhispania mnamo Mei 2021.

Mnamo 2020, Sancho ambaye kwa sasa amehamia Man-United kutoka Borussia Dortmund ya Ujerumani, alikuwa miongoni mwa wanasoka waliolalamikia pakubwa tukio la George Floyd kuuawa na afisa wa polisi mjini Minneapolis, Amerika.

Mwanasoka mwingine wa Uingereza ambaye amekuwa akikabiliana mara kwa mara na matukio ya kubaguliwa kirangi ni fowadi Raheem Sterling wa Manchester City.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mrengo wa tatu wa kisiasa waibuka Bondeni

MKU yashirikiana na UN kuwajali wanaoishi na ulemavu