Habari Mseto

Facebook kutua Nairobi kuvumisha huduma zake kwa Kiswahili

February 11th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

KAMPUNI ya huduma za mitandao ya kijamii Facebook inalenga kufungua afisi za huduma zake Jijini Nairobi, kama mbinu ya kupanua biashara barani Afrika na kuboresha huduma kwa wateja wake.

Kulingana na taarifa, kampuni hiyo itashirikiana na ile ya Samasource ambayo ni ya kidijitali na ambayo ina umaarufu Afrika Mashariki.

Kufikia mwishoni mwa mwaka 2019, Facebook inatarajia kuwaajiri watu 100 kufanya kazi ya ukaguzi wa mitandao yake.

Wakaguzi hao watawezesha mitandao ya kampuni hiyo kuwezesha lugha za Kiswahili, Somali, Oromo, na Hausa kutumika, kama mbinu ya kuwavuta wazungumzaji wa lugha hizo ndani yake zaidi.

“Tunataka Facebook kuwa mahali ambapo watu wanaweza kujieleza na kujadili kwa njia huru masuala tofauti yanayowahusu, huku tukihakikisha kuwa ni mahali salama kwa kila mtu,” akasema Fazdai Madzingira, afisa wa kampuni hiyo.

Kuleta afisi hizo Nairobi ni sehemu ya lengo la Facebook kuzidi kuwekeza barani Afrika, Bw Ebele Okobi, Mkurugenzi wa ukaguzi wa umma katika kampuni hiyo akasema.

Maafisa hao walisema kuwa kufungua afisi hizo kutawezesha kampuni ya Facebook kuanza kukagua jumbe ambazo zinachapishwa katika mtandao wake kutoka barani kwa mara ya kwanza.