Kimataifa

Facebook yamzima mwanawe Netanyahu kutaka Waislamu watimuliwe Israeli

December 20th, 2018 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

YAIR Netanyahu, mwanawe Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Jumapili alipigwa marufuku katika mtandao wa Facebook kwa muda, baada ya kuweka chapisho lililokosoa mtandao huo wa kijamii kuwa ni “askari wa akili.”

Hii ilikuwa baada ya mtandao huo wiki iliyopita kuondoa chapisho la Bw Netanyahu jingine wiki iliyopita, ambapo alikuwa anapendekeza Waislamu wote kuondoka Israel.

Mbeleni vilevile, Bw Netanyahu alitumia mtandao huo kuapa ‘kulipiza kisasi vifo’ vya wanajeshi wawili wa Israel ambao waliuawa wiki iliyopita na wapiganaji wa Palestine. Facebook iliondoa chapisho hilo.

Kijana huyo wa miaka 27 alikuwa ametumia chapisho hilo kutaka raia wote wa Palestine kupigwa marufuku Israel.

Mnamo Jumapili, alichapisha picha za simu za machapisho ambayo Facebook ilikuwa imeondoa mtandaoni kwani yalikuwa yamekiuka kanuni zake. Muda mfupi baadaye, alipigwa marufuku na mtandao huo kwa saa 24.

Kijana huyo hajakuwa mgeni kwa visa vya kutatanisha, kwani mara kwa mara amekuwa akifanya mambo ya aibu, hata wakati mwingine ikimlazimu babake kuingilia kati.

Mnamo Januari, Waziri huyo Mkuu wa Israel alilazimika kujitokeza kumtetea mwanaye, baada yake kurekodiwa akitumia matamshi mabaya kuhusu wanawake na kujisifu kwa marafiki zake namna anapenda makahaba.

Katika sauti hizo za kurekodiwa ambazo zilichezwa na kituo kimoja cha runinga nchi hiyo, kijana huyo wa Waziri Mkuu alikuwa akijisifu kwa mwanawe tajiri mmoja wa mafuta, ambaye alimwambia kuwa babake (Netanyahu) alimsaidia babake rafiki huyo kupata mradi wa dola 20bilioni bungeni.

Rekodi hiyo ilisababisha kelele kote Israel, na baadaye wote baba na mtoto wakajitokeza kutoa maneno ya kuwatuliza raia wan chi hiyo.

Kijana huyo aidha amekuwa akikashifiwa na watu wan chi hiyo kwa kujionyesha namna anavyoishi maisha ya kifalme katika mitandao ya kijamii.