Makala

Fahamu athari za mvua ya theluji Kinangop

February 1st, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

ENEO la Kinangop linafahamika kama mojawapo ya maeneo yenye baridi kali zaidi nchini.

Kuna wale huliita eneo hilo lililo katika Kaunti ya Nyandarua kama ‘Amerika ya Kenya’ kutokana na hali ya baridi kubwa iliyo katika eneo hilo.

Majuzi, eneo hilo lilikumbwa na mvua kubwa, ambapo kando na kuharibu barabara, ilisababisha msururu wa theluji zilizokaa siku mbili bila kuyeyuka kutokana na kiwango cha chini cha joto.

Kwenye mahojiano, wenyeji wa eneo hilo wanataja ukaribu wake na milima ya Aberdares kama sababu kuu ya uwepo wa kiwango cha juu cha baridi.

“Eneo hili linapakana moja kwa moja na Milima ya Aberdares. Ni eneo lenye miinuko na miti mingi na mikubwa sana. Hiyo ndiyo hali ambayo bila shaka imechangia kiwango cha baridi kwa karibu kila msimu wa mwaka,” asema Bi Charity Wangui, ambaye ni mkazi.

Licha ya kuwa mkazi wa eneo hilo kwa zaidi ya miaka 20, Bi Wangui alisema alikumbwa na mshtuko mkubwa alipoona mvua ya theluji ikinyesha katika eneo hilo, na theluji hizo kukaa siku kadhaa kabla hazijayeyuka.

“Huu ulikuwa mshangao mkubwa sana kwangu. Hiki kilikuwa kioja ambacho sijawahi kukiona maishani mwangu. Haya ni mambo ambayo huwa nayaona kwenye mitandao ya intaneti na kwenye sinema au filamu,” akasema Bi Wangui.

Wakazi wengine waliozungumza na Taifa Leo walitoa kauli kama hizo.

Hata hivyo, licha ya mvua hiyo kuwa baraka kwa wenyeji, baadhi yao walilalamikia uharibifu wake mkubwa, kwani ilimlazimu Naibu Rais Rigathi Gachagua kufika katika eneo hilo kwa dharura kuwasaidia waathiriwa wa mvua hiyo.

Zaidi ya hayo, walisema kuwa athari zake nyingine zilikuwa uharibifu mkubwa wa barabara, kwani baadhi yazo hazikuwa zikipitika.

Baadhi ya mazao, kama vile mboga, pia yaliharibiwa vibaya.

“Mvua ni baraka. Uwepo wa theluji pia lilikuwa tukio la kipekee kwa baadhi ya watu, kwani hawajawahi kuziona. Hata hivyo, ilisababisha uharibifu mkubwa,” akasema Bw Maina Wambugu, ambaye ni mkazi.

Alisema ilikuwa vigumu kwa magari kutumia baadhi ya barabara kwa sababu theluji hizo zililala kama zulia.

Pia vigingi vya stima viliangushwa na mvua hiyo.

Kigingi cha stima kilichoangushwa na mvua ya theluji. PICHA | WANDERI KAMAU

Alipofika eneo hilo Jumanne, Bw Gachagua alisema kuwa licha ya uharibifu huo kutokea, ana furaha kwamba hakuna maafa wala majeraha yoyote yaliyotokea.

“Nimefika hapa kuwafariji waathiriwa wa uharibifu huu. Nawapa pole wale wote walioathiriwa. Haya yanatokana na mabadiliko ya hali ya hewa, japo kama serikali tunaendesha juhudi za upanzi wa miti ili kudhibiti madhara kama hayo,” akasema Bw Gachagua.

Wazee wachache walisema eneo hilo linafaa kutangazwa kama la kipekee nchini kutokana na ‘kioja’ hicho kwao.

Theluji ikiwa imefunika shamba la miti katika eneo la Kinagop majuzi. PICHA | WANDERI KAMAU