Lugha, Fasihi na Elimu

Fahamu jinsi mwalimu huyu anavyotumia ubunifu katika ufundishaji

May 14th, 2024 2 min read

WANAFUNZI wanahitaji mazoezi mengi iwezekanavyo ili wajiamini katika ujifunzaji wa dhana mpya.

Njia rahisi ya kukuza uwezo wao wa kuhusisha wanachokisoma darasani na matukio halisi na ya kawaida katika jamii ni kuwashirikisha katika masuala yanayohitaji ubunifu wa kiteknolojia.

Pamoja na kutumia vifaa vya kidijitali ambavyo husisimua wanafunzi, matumizi ya video, michoro na picha za rangi ni namna nyingine ya kufanya shughuli za ujifunzaji ziwe za kuvutia.

Michezo, nyimbo na mashairi mepesi ambayo wanafunzi wanaweza kuimba kwa urahisi pia yatamsaidia mwalimu kufikia malengo hayo.

Haya ni kwa mujibu wa Bw Martin Ekaliani ambaye kwa sasa ni Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi ya St Peter The Apostle Catholic iliyoko Lower Kabete, Kaunti ya Kiambu.

“Mwanafunzi akipata umilisi na ujuzi unaofaa, atakuwa wa manufaa makubwa katika jamii ya sasa inayoshuhudia mabadiliko ya kasi kiteknolojia,” anakiri.

Kutokana na ukweli huu, ipo haja kwa walimu kukumbatia matumizi ya mbinu za ufundishaji zitakazompa mwanafunzi nafasi murua za kutambua mwegemeo wa talanta zake.

“Kuhusisha wanafunzi moja kwa moja katika masomo yanayohitaji ubunifu wa kiteknolojia kunawapa fursa ya kufanya mambo kwa kujiamini. Mawanda ya fikira zao hupanuka, uelewa wao huimarika na huanza kuona vitu wanavyofundishwa vikiwa vya kawaida mno,” anasema.

“Hali hii huchochea bongo zao kufanya kazi na hatimaye maarifa wanayochota vitabuni na kutoka kwa walimu wao huamsha hamu ya uvumbuzi ndani yao,” anaelezea.

Kwa mtazamo wake, uzuri wa kufundisha watoto wa umri mdogo – wa kiwango cha chekechea, shule za msingi na sekondari msingi (JSS) – ni kwamba wanaelewa mambo upesi na wana hamu ya kujifunza vitu vipya kila mara.

Martin alilelewa katika eneo la Kiwanja Ndege, Sinoko, Kaunti ya Bungoma.

Ndiye wa nne kuzaliwa katika familia ya watoto sita wa marehemu Bw Johnstone Aunyasi Ole na marehemu Bi Marciana Adionyi.

Safari yake ya elimu ilipitia katika Shule ya Msingi ya Bungoma DEB (1984-1991) na Shule ya Upili ya St Peter’s Mumias Boys (1992-1995).

Alipokea mafunzo ya kompyuta katika Institute of Advanced Technology, Nairobi (1996-1998) kabla ya kusomea masuala ya bima na biashara katika College of Insurance, South C, Nairobi (1997-1998).

Maarifa hayo yalimpa fursa ya kuwa mkufunzi wa kozi za kiteknolojia katika Gateway Computer College, Bungoma (2002-2003).

Ingawa alitamani kujitosa katika tasnia ya uanahabari, alihiari baadaye kusomea taaluma ya ualimu katika Chuo cha Mafunzo ya Walimu cha Eregi, Vihiga (2003-2004).

Alianza kufundisha katika Shule ya Msingi ya Marell Academy Bungoma na akahudumu huko kati ya 2005 na 2008 akiwa Mkuu wa Idara ya Lugha.

Alihamia baadaye jijini Mombasa kuwa Mkuu wa Idara ya Kompyuta na Michezo wa The Nyali School (2009-2012) kabla ya kuajiriwa kuwa Mwalimu Mwandamizi katika Shule ya Msingi ya MM Shah, Mombasa (2012-2020). Martin amewahi pia kufundisha Nairobi School Primary & JSS (2021-2023).

Mkewe wa kwanza, Bi Ann Odinga Akoolo, aliaga dunia mnamo 2014 wakiwa na watoto wawili – Mercellus na Marciana.

Kwa pamoja na mkewe wa sasa, Bi Valeria Mghana, wamejaliwa mtoto, Briel. Bi Mghana ni mwalimu katika Shule ya Kimataifa ya Mudzini, Kilifi.