Makala

Fahamu mbinu rahisi ya kutambua kama kaa ni jike au dume

March 13th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

VYAKULA vya baharini, mitoni na katika maziwa mara nyingi vinaaminika kuwa na faida kuliko vile vipatikanavyo nchi kavu.

Ni kutokana na hilo ambapo utasikia waja wakijibizana au kukagua na kukimbilia kupendelea mlo wa nyama nyeupe badala ya nyekundu.

Mara nyingi nyama nyeupe hupatikana kwa samaki na viumbe wengine wa baharini au majini ilhali nyama nyekundu ikipatikana kwa wanyama wa nchi kavu kama vile ng’ombe, nguruwe, kondoo, mbuzi, sungura na wengineo, hasa wale wote wenye miguu minne.

Kwa wapenzi wa vyakula vya baharini, mito na maziwa, ni dhahiri kuwa lazima unajua au kuwahi kula viumbe kama vile kaa, pweza, samaki, kambakoche na wengineo.

Kwa watalii na wageni wanaozuru Pwani ya Kenya, ikiwemo Lamu, Malindi, Kilifi, Mombasa na Kwale, mara nyingi utasikia wakiitisha mezani vyakula vya baharini, hasa kaa ili wafurahie mlo huo wanaoamini kuwa na utajiri mkubwa wa virutubisho halisi, hasa protini.

Protini ni kirutubisho cha kujenga mwili na kuupa ngunvu kilichopo kwa vyakula kama vile nyama na samaki ambacho ni mchanganyiko wa kaboni, hidrojeni,, oksijeni, nitrojeni, chuma nakadhalika.

Licha ya wengi kufahamu fika kwamba viumbe hawa wana jinsia ya kike na kiume, ni vigumu kwao kuingia mkahawani na kisha kuitisha mlo wa kaa au pweza wa kiume au kike.

Kaa dume na kaa jike

Lakini je, unajua kwamba zipo mbinu bayana za kutofautisha baina ya kaa dume na jike?

Kulingana na maelezo ya kimsingi ya kamusi, kaa ni mnyama mdogo wa majini mwenye miguu sita au zaidi na gamba mwilini.

Wavuvi wa Lamu waliobobea kwenye nyanja hiyo ya uvuvi waliotangamana na mwandishi wa Taifa Leo walifafanua na hata kuonyesha jinsi wao kwa miaka mingi wamefaulu kumtambua au kumbainisha kaa mke na mume kienyeji.

Cha kufurahisha na kutia au kujenga imani zaidi ni kwamba baadhi ya mbinu wanazotumia wavuvi hao asilia wa Lamu kumtofautisha kaa jike na dume pia zimekaguliwa, kuhakikiwa na kupasishwa kitaalamu au kisayansi ulimwenguni.

Bw Swaleh Abdalla, mvuvi kisiwani Pate, Lamu Mashariki, akionyesha kaa wa kiume. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Swaleh Abdalla, mvuvi kutoka kisiwa cha Pate, Lamu Mashariki, anasema ili kumtofautisha kaa jike na dume, wao hulazimika kuwapindua na kuwatazama sehemu yao ya tumbo kwa chini.

Kulingana na Bw Abdalla, kuna umbo, mchoro au duara maalumu kwenye sehemu ya tumbo la kaa ambalo ni kibainishi tosha cha kaa mke na mume.

“Hapa utapata umbo, mchoro au mduara wa kaa mume ulioko chini ya tumbo lake ni mwembamba ilhali yule kaa wa kike, umbo au duara lake chini ya tumbo likiwa pana na linaloshabihiana na duaradufu,” akaeleza Bw Abdalla.

Bw Swaleh Abdalla, mvuvi kisiwani Pate, Lamu Mashariki, akionyesha kaa wa kike. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Mohamed Hassan, mvuvi tajika wa kaa wa matope Lamu, anasema kwa walaji kaa ambao huenzi sana jinsia ya kiume hawana haja ya kubahatisha, kupapatika au kutapatapa.

Bw Hassan anasema mbali na kutambua jinsia ya mnyama huyo kupitia umbo au mduara wa chini ya tumbo, pia kuna mbinu nyingine tele za kubainisha jinsia ya kaa.

Anataja saizi kuwa miongoni mwa vigezo vya kutofautishia kaa wa kiume na kaa wa kike.

Anasema mara nyingi kaa dume huwa kipimo au saizi yake ya mwili na mikono anayotumia kukamatia lishe lake ni kubwa ilhali yule wa kike akiwa na tumbo kubwa lakini sehemu nyingine za mwili wake kwa ujumla zikiwa ndogo.

Bw Hassan aliongeza kuwa mikono ya kaa dume anayokamatia chakula huwa mara nyingi ni ya rangi ya samawati au bluu ilhali kaa jike mikono yake ikiwa rangi nyekundu iliyokatikakatika.

“Sisi hatutapitapi hapa Lamu mteja anapotuambia tumvulie baharini au kumpakulia hotelini kaa dume au jike. Twajua kaa dume ni mkubwa wa mwili ilhali jike akiwa mdogo na kitumbo kikubwa. Pia twangalia rangi ya mikono yak aa. Buluu au samawati yaashiria huyo ni kaa mume ilhali nyekundu iliyokoleza mahali mahali ikiashiria kaa mke,” akasema Bw Hassan.

Bi Tima Omar, mvuvi mwanamke eneo la Kiunga mpakani mwa Kenya na Somalia anasema uzito wa kaa pia hutumika kutofautisha yupi mwanamke na ni yupi mwanamume.

Kulingana na Bi Omar, kaa wanaume huwa na uzito mkubwa, ikizingatiwa kuwa mwili wao mara nyingi huwa mkubwa.

Hiyo ni tofauti na uzito wa kaa mwanamke ambaye huwa hafifu kutokana na kwamba kwa kawaida mwili wake huwa saizi ndogo.

“Ukichunguza tabia za wanyama hawa pia utatofautisha jinsia zao kiurahisi. Kwa mfano, kaa mume mara nyingi huanzisha vita vya kuonyesha ubabe, hasa anapomuona kaa mke ambaye ana mikono mikubwa kumshinda. Licha ya hayo, kaa huyo mke mwenye mikono mikubwa huwa hajitetei anapovamiwa bali husalia kupigwa na kaa dume hata kama ni mdogo,” akasema Bi Omar.

Wavuvi wa Lamu pia wanasema kaa wanawake mara nyingi ndio wenye tabia ya kutulia kulea (tabia ya malezi au uzazi), ikiwemo kuwakinga kaa wadogo kutokana na hatari kwenye mazingira waliyotagiwa na kukulia ndani.

Tabia hiyo ni kinyume kabisa kwa kaa dume ambao mara nyingi hujitia hamnazo kimajukumu ya malezi.