Habari za Kaunti

Fahamu msikiti maridadi zaidi kisiwani Lamu

February 9th, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

KISIWA cha Lamu ambacho ni ngome ya dini ya Kiislamu kina zaidi ya misikiti 40 inayopatikana kwenye maeneo au mitaa mbalimbali.

Kisiwa hicho kinajumulisha Mji wa Kale wa Lamu, ule wa Shella, Wiyoni, Kashmir, Kandahar, Bombay, Makafuni na Matondoni.

Mji wa Kale wa Lamu, ambao ndio kitovu cha Uislamu katika Ukanda wa Afrika Mashariki umedumu kwa zaidi ya miaka 700.

Ni kwenye kisiwa hicho ambapo utapata misikiti mikongwe zaidi ambayo imedumu kwa kati ya miaka 100 na hata 600.

Aidha ni kisiwani Lamu ambapo utapata misikiti iliyorembwa ikarembeka si haba.

Mmoja wa misikiti inayotambuliwa kuwa maridadi zaidi kisiwani Lamu ni ule wa Riyadha.

Msikiti huo mrembo, mpambe au maridadi unapatikana mtaa wa Riyadha ambao uko katikati au kitovuni mwa Mji wa Kale wa Lamu.

Licha ya kuwa miongoni mwa maabadi ya jadi zaidi yapatikanayo kisiwani Lamu, Msikiti wa Riyadha huonekana kuwa maridadi kila kukicha, hasa kutokana na umbo lake la nje ambalo ni lenya mvuto wa kipekee.

Isitoshe, ni msikiti huo ambao kila mara utawapata wenyeji au waumini wakiwa wameurembesha, iwe ni kwa vitambaa vya rangi aina aina au kuupaka rangi zake za kijani na nyeupe zilizokoleza.

Msikiti wa Riyadha. PICHA | KALUME KAZUNGU

Aghalabu anayefika kwenye msikiti wa Riyadha atakubali au kusalimu amri kwamba kwa kweli ni wenye kuvutia, iwe ni kwa nje au ndani.

Je, msikiti huo ulianzishwa lini na ni nani mwanzilishi?

Kulingana na Katibu Mkuu wa Msikiti huo uliojumuisha chuo maarufu na tajika cha Mafundisho ya Dini ya Kiislamu Afrika Mashariki cha Riyadha, Bw Abubakar Badawy, msikiti huo una zaidi ya miaka 120 eneo hilo.

Bw Badawy anafichua kuwa mwanzilishi wa msikiti huo, ambao pia umeorodheshwa na Halmashauri ya Makavazi na Turathi Nchini (NMK) kuwa makavazi ya kihistoria, ni Bw Habib Swaleh.

Bw Habib Swaleh ni msomi anayeaminika kuweka mizizi ya dini ya Kiislamu kisiwani Lamu na kusaidia ikaenea Afrika Mashariki.

Nyumba ya mwanzilishi wa msikiti wa Riyadha na kituo cha mafunzo ya dini, Habib Swaleh, kwenye uwanja wa msikiti wa Riyadha mjini Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Mbali na umaridadi wa jengo la msikiti wa Riyadha, pia unapofika kwenye uwanja wa msikiti huo utakaribishwa na mandhari ya ukale kwani nyumba ya udongo alimoishi Bw Habib Swaleh bado ipo ikiwa imesimama tisti pembezoni mwa uwanja.

Bw Badawy anashikilia kuwa babu yake, Habib Swaleh ndiye aliyeanzisha msikiti wa Riyadha pamoja na chuo chake maarufu kwa mafundisho ya dini ya Kiislamu.

“Babu Habib Swaleh kwanza alianza kwa kujenga nyumba hii ya udongo. Nyumba hii imesalia kuwa maonyesho ya wageni wanaotembelea Lamu na msikiti kujua historia yake. Nyumba na msikiti tunaamini vyote vimedumu hapa kwa zaidi ya miaka 120 sasa,” akasema Bw Badawy.

Wanaotembelea nyumba ya Habib Swaleh hupata fursa ya kujifunza maisha ya utawa aliyokuwa akiishi msomi, mdini na mwanachuoni huyo kabla ya kifo chake mwaka 1935.