Makala

Fahamu mwalimu anayetumia TikTok kunoa wanafunzi wake  

April 15th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

MFUMO mpya wa Elimu ya Umilisi na Utendaji (CBC) unasisitiza kuhusu umuhimu wa wanafunzi kuwa na uelewa wa ujuzi utakaowasaidia katika maisha yao ya baadaye.

Hili ni kinyume na mfumo wa 8-4-4, uliojikita sana katika masuala ya mitihani, na gredi ambayo mwanafunzi husika angepata.

Katika kukumbatia na kuendeleza lengo kuu la mfumo wa CBC, mwalimu Christine Mulekye Mwilu, ameegemea katika matumizi ya mtandao wa TikTok, kuhakikisha kuwa wanafunzi wake wanaelewa yale anayowafunza.

Mwalimu Christine, kama anavyofahamika na wanafunzi wake, anahudumu katika Shule ya Msingi ya Kibinafsi ya Maramat, iliyo katika eneo la Ngong, Kaunti ya Kajiado.

Je, ni nini kilimsukuma kukumbatia matumizi ya mtandao wa TikTok licha ya maovu ambayo yamekuwa yakihusishwa na mitandao ya kijamii?

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Dijitali, mwalimu huyu anasema kuwa nyakati zimebadilika, hivyo ni wakati walimu watambue kwamba pia wanawafunza wanafunzi wa kizazi tofauti na vizazi vya hapo nyuma.

“Nyakati zimebadilka. Teknolojia kwa sasa ndiyo njia kuu ya kutoa mafunzo kwa wanafunzi. Ujio wa mitandao ya kijamii umebadilisha kabisa utoaji mafunzo kwa wanafunzi,” asema Mwalimu Christine.

Kulingana naye, matumizi ya mtandao wa TikTok yameleta mabadiliko na mwamko wa kipekee miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake, ambao awali walionyesha tashwishi kuhusu ikiwa juhudi zake zingefaulu.

“Nilianza matumizi ya TikTok kuwafunza wanafunzi wangu Agosti 11, 2023. Hili ni baada ya video moja iliyowekwa katika mtandao huo, iliyomwonyesha mwalimu akimchapa vibaya na kumdhulumu mwanafunzi mchanga. Video hiyo iliwasawiri vibaya walimu. Ni jambo lililonikera sana, japo lililonihamasisha kubuni njia ambayo ninaweza kubadilisha dhana kuhusu walimu kwa kutumia mitandao ya kijamii,” akasema.

Mwalimu Christine alizaliwa katika Kaunti ya Kitui.

Alisomea katika Shule ya Msingi ya Matinyani DEB. Baadaye, alielekea katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Matinyani, iliyo katika kaunti iyo hiyo. Baada ya masomo yake ya sekondari, alijiunga na Chuo cha Walimu cha Kitui, alikosomea ualimu kati ya 2012 na 2014.

Tangu wakati huo, amesomesha katika shule kadhaa, hadi sasa ambapo ameamua kujiunga na Chuo Kikuu cha Mt Kenya kusomea Shahada ya Ualimu katika masomo ya Jiografia na Kiswahili.

Kwenye juhudi zake za kukumbatia mitandao ya kijamii kunoa wanafunzi, haijakuwa safari rahisi.

Anasema baadhi ya wazazi bado wana mitazamo ya kizamani, hivyo huwa hawaelewi umuhimu na maana ya matumizi ya teknolojia kuwafunzia watoto.

“Ili kuepuka changamoto hiyo, tumeanza mpango maalum wa kuwahamasisha wazazi na jamii nzima kwa jumla kuhusu umuhimu wa kukumbatia teknolojia, japo kwa kuzingatia tahadhari,” akasema.

Akaunti yake ya TikTok ni: Teacher Christine. Pia, anatumia mtandao wa YouTube, anakojiita vivyo hivyo.

Wito wake kwa walimu kote nchini ni kukumbatia matumizi ya teknolojia kuwafunzia wanafunzi.