Makala

Fahamu sababu za upole wa punda wa Lamu

February 23rd, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

KAUNTI ya Lamu inavuma kwa kuwa na idadi kubwa ya mnyama punda.

Punda ndio ambao tangu jadi wamekuwa wakitumika kwa shughuli za kila siku za uchukuzi, hasa kwenye maeneo ya visiwani ambako hakuna magari na mbinu nyingine zozote za kisasa za uchukuzi, ikiwemo pikipiki na baiskeli.

Lamu ina zaidi ya visiwa 35 vipatikanavyo kwenye maeneo tofautitofauti.

Mbali na kisiwa cha Lamu, pia kuna Kizingitini, Pate, Mtangawanda, Mkokoni, Kiwayu, Ndau, Siyu, Shanga, Rubu, Faza na vinginevyo vingi, ambapo usafiri wa kutegemewa hapa ni hawa punda.

Wengi wanaposikia punda akitajwa, kinachowajia haraka akilini ni sifa za mnyama huyu kuwa na mateke au mapigo makali ya mguu ambayo ni yenye kuumiza.

Ndipo wahenga wakaja na methali kuwa ‘Asante ya Punda ni Mateke’.

Lakini kwa upande wa sifa za punda wa Lamu, methali hii ni kinyume kabisa.

Punda wa kaunti ya Lamu wanatambulika kwa kuwa wapole na utaratibu wenye mvuto.

Kinyume na punda wa Nakuru, Kilifi, Turkana, Marsabit, Isiolo, Machakos, Makueni na kwingineko ambapo kumkaribia punda ni sawa na kuhatarisha maisha kwani huenda ukapigwa mateke ya kufisha, Lamu utampata mwenye punda akimbusu mnyama wake, kumparamia mgongoni na kuchezacheza naye kwa kumshika miguu na kwato bila ya uoga wowote.

Yaani punda wa Lamu na binadamu ni sawa na simulizi za Kurwa na Doto.

Lakini je, ni nini hasa ambacho punda wa Lamu hufanyiwa, hivyo kujenga au kuwa wapole namna hiyo?

Mmoja wa wamiliki mashuhuri wa punda kisiwani Lamu, Bw Hussein Miji, anataja hulka ya upole wa punda wa Lamu kwamba unatokana na ukarimu na matunzo ambayo wenye punda wameyadumisha kwa wanyama wao.

Punda wakiwa wamebeba makuti kisiwani Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Miji anasema kinyume na maeneo mengine ya Kenya na ulimwengu ambapo punda hubaguliwa au kufugwa katika hali sawia na mnyama mwitu, wamiliki wa punda Lamu wamejenga na kudumisha ukaribu zaidi na wanyama wao.

Anasema ni Lamu ambapo punda hutumiwa katika hali ya moja kwa moja, ikiwemo kupandwa mgongoni kinyume na sehemu zingine za nyi na ulimwengu ambapo lazima punda kusukuma kigari cha magurudumu nyuma kinachotumiwa kubeba mizigo.

Bw Miji pia anataja jinsi punda wanavyochukuliwa au kutunzwa Lamu, ikiwemo chakula wanachopewa, kuogeshwa na mahitaji mengine kuwa kigezo tosha kinachowafanya wanyama hao kuwa wapole kushinda punda wa maeneo mengine yoyote ya nchi na ulimwengu.

“Ukitazama, ni Lamu pekee ambapo utampata mwenye punda akimuogesha punda wake baharini. Kinyume na sehemu zingine ambapo chakula cha punda ni nyasi pekee, hapa Lamu utapata punda akilishwa wishwa na vyakula vingine. Pia utapata mwenye punda akimpakulia mnyama wake ugali, mchele, mikate na vyakula vingine ilmradi aonyeshe mapenzi kwa punda wake. Ukarimu huo ndio unaowafanya punda wa Lamu kuwatii mabwana zao na kuwa wapole kabisa,” akasema Bw Miji.

Bw Mohamed Abeid, mmoja wa wamiliki wa punda eneo la Pamba Roho kisiwani Lamu, anasema upole wa punda wa eneo hilo pia unatokana na jinsi ambavyo punda wamepewa malezi bora na pia kufugwa kwenye mazingira ya kutangamana na binadamu mapema, tangia kuzaliwa, kukua na kuzeeka kwao.

Bw Mohamed Abeid ambaye anamiliki punda mtaani Pamba Roho kisiwani Lamu. Anampiga pambaja punda wake. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Abeid anasema ni kutokana na hilo ambapo punda hawashtuki kumuona binadamu wakiwakaribia.

“Punde punda anapojihisi kuhatarishwa kimaisha, hapo ndipo hurusha mateke. Lakini hapa wa Amu wametambua siri mapema. Wamedumisha utu na mapenzi yao kwa punda. Punda wanapokaribia binadamu hujihisi salama na hawana la kuwasukuma kurusha mateke,” akasema Bw Abeid.

Afisa wa Maslahi ya Punda katika kituo cha Matibabu ya Punda cha Lamu Obadiah Sing’oei alikinzana na wahenga wanaodai asante ya punda ni mateke.

Bw Sing’oei aliwasifu wakazi wa Lamu, hasa wale wanaozingatia kuheshimu haki za punda akisema ni kutokana na hilo ambapo waja hao hata hawafahamu usemi au sifa za punda na mateke.

“Punda ukimtunza atakutunza hata zaidi. Wale wanaosema asante ya punda ni mateke nahisi wanakosea. Vile utakavyomchukulia punda ndiyo vile ambavyo naye atakuchukulia. Ningewahimiza watu kuwaangalia vyema punda wao kwa kuwapa malezi bora, chakula, mazingira bora ya kuishi, matibabu bora, mapumziko nakadhalika. Ninaamini wakifanya hivyo punda hao watawatunza vyema na wala hakutakuwa na mateke yanayodaiwa,” akasema Bw Sing’oei.