Makala

Fahamu uhusiano wa matumizi ya simu na Kansa ya ubongo

Na BENSON MATHEKA September 6th, 2024 1 min read

HAKUNA uhusiano kati ya matumizi ya simu za rununu na kuongezeka kwa hatari ya Saratani ya ubongo, kulingana na uchunguzi mpya wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Licha ya ongezeko kubwa la matumizi ya teknolojia isiyotumia waya, hakujawa na ushahidi kwamba yanasababisha ongezeko sawa la matukio ya Saratani ya ubongo, ripoti iliyochapishwa Jumanne, Septemba 3, 2024 ilisema.

Hii ni hata kwa watu wanaopiga simu kwa muda mrefu au wale ambao wametumia simu za mkononi kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Uchambuzi wa mwisho ulijumuisha tafiti 63 kutoka 1994-2022, zilizotathminiwa na wachunguzi 11 kutoka nchi 10, ikiwa ni pamoja na mamlaka ya ulinzi wa miale ya serikali ya Australia.

Utafiti huo ulitathmini athari za masafa ya redio, yanayotumiwa katika simu za rununu na vile vile runinga. “Hakuna lililoonyesha hatari zaidi,” walisema watafiti. Uchunguzi uliangazia Saratani za ubongo kwa watu wazima na watoto, pamoja na Saratani ya tezi zikiwemo za mate na damu (leukemia), na hatari zinazohusiana na matumizi ya simu za mkono.

Awali, WHO na mashirika mengine ya afya ya kimataifa yalisema hakuna ushahidi wa uhakika wa madhara ya kiafya kutokana na matumizi ya simu za mkononi, lakini ilitaka utafiti zaidi.