Michezo

FAHARI TELE: Historia mataifa yote ya Afrika Mashariki kutua fainali AFCON

March 26th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

DAR ES SALAAM, TANZANIA

TANZANIA waliwapepeta Uganda 3-0 jijini Dar es Salaam mnamo Jumapili na kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980.

Taifa Stars walihitaji ushindi katika mchuano huo wa mwisho katika Kundi L ili kuungana na Uganda katika safari ya kuelekea Misri kwa ajili ya fainali zitakazofanyika kati ya Juni na Julai 2019.

Lesotho waliambulia sare tasa dhidi ya Cape Verde katika mchuano mwingine uliowashuhudia wakibanduliwa kwenye Kundi L.

Ufanisi wa Tanzania una maana kwamba mataifa manne kutoka Afrika Mashariki – Tanzania, Uganda, Burundi na Kenya yatanogesha fainali za AFCON mwaka huu nchini Misri.

Baadhi ya mashabiki wa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’. Picha/ Hisani

Uganda walishuka dimbani kuchuana na Tanzania wakijivunia rekodi ya kutofungwa bao lolote katika kampeni zao za kufuzu kwa fainali za AFCON muhula huu.

Hata hivyo, rekodi hiyo ilifutwa katika mechi yao ya sita baada ya Simon Msuva kumzidi maarifa kipa Denis Onyango na hivyo kuwafungulia Tanzania ukurasa wa mabao kunako dakika ya 21.

Erasto Nyoni aliongeza bao la pili baada ya mapumziko huku Aggrey Morris akizamisha kabisa chombo cha Uganda mwishoni mwa kipindi cha pili.

Hata hivyo, Tanzania wangaliambulia patupu licha ya ushindi huo mnono iwapo Lesotho wangaliwazidi maarifa Cape Verde katika mchuano mwingine wa Kundi L jijini Praia.

Karibu miongo minne nje

Chini ya kocha Emmanuel Amunike ambaye ni winga wa zamani wa Super Eagles ya Nigeria, Taifa Stars kwa sasa watashiriki fainali za AFCON kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39.

Kwingineko, Khama Billiat na Knowledge Musona walifunga mabao muhimu yaliyowapa Zimbabwe tiketi ya kufuzu kwa AFCON baada ya kuwapepeta Congo.

Zimbabwe walijibwaga kwa mchuano huo wakihitaji sare ya aina yoyote ili kuweka hai matumaini ya kufuzu. Kwa upande wao, Congo walikuwa na ulazima wa kusajili ushindi na kujizolea alama zote tatu ili kujikatia tiketi ya kushiriki AFCON kwa mara ya kwanza tangu 2015.

Bafana Bafana ya Afrika Kusini pia walifuzu kwa fainali za AFCON baada ya kuwapepeta Libya 2-1 katika uwanja wa Taieb Mhiri jijini Sfax.

Wakihitaji sare ya aina yoyote ili kufuzu, Afrika Kusini walifungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Percy Tau kunako dakika ya 50.

Ahmad Benali aliwarejesha Libya mchezoni kupitia mkwaju wa penalti kunako dakika ya 66 na kuwazidishia wageni wao presha.

Ingawa hivyo, Tau alipachika wavuni bao la pili la Afrika Kusini kunako dakika ya 69 na kuwahakikishia Afrika Kusini ushindi uliowawezesha kuungana na Nigeria katika kilele cha Kundi E.

Vikosi vingine ambavyo tayari vimefuzu kwa fainali za AFCON 2019 ni pamoja na Ivory Coast, Madagascar, Mali, Mauritania, Morocco, Algeria, Nigeria, Cameroon, Ghana, Guinea, Angola, Senegal, Namibia na wenyeji Misri.

Burundi walifuzu kwa mara ya kwanza katika historia ya kipute cha AFCON baada ya kuwalazimishia Gabon sare ya 1-1 jijini Bujumbura.

Cedric Amissi aliwafungia Burundi bao kunako dakika ya 76.

Hadi waliposhuka dimbani kwa minajili ya kipute hicho, Burundi walikuwa wakihitaji sare ya aina yoyote ili kujikatia tiketi ya kushiriki fainali za AFCON nchini Misri mnamo Juni 2019.

Ingawa Omar Ngando alijifunga kunako dakika ya 82, hilo halikutosha kuwapa Gabon waliojivunia huduma za fowadi Pierre-Emerick Aubameyang hamasa ya kupata goli la pili na la ushindi.

Matokeo hayo yaliwasaza Burundi waliokuwa na Saido Berahino wa Stoke City na Gael Bigirimana wa Hibernia, katika nafasi ya pili kwenye Kundi C ambalo linaongozwa na Mali.

Gabon ambao walikuwa wenyeji wa fainali za 2017, wanashikilia nafasi ya tatu.