Pambo

Faida za ndimu si jikoni pekee bali hata kwa urembo

April 6th, 2024 2 min read

NA PAULINE ONGAJI

NDIMU hutumika hasa jikoni kwa mapishi na hata usafi.

Lakini je, wajua kwamba hata katika masuala ya urembo na mwonekano, tunda hili lina faida tele?

Hasa katika enzi hizi ambapo mabinti wanafanya kila juhudi kuimarisha mwonekano wao, wanapaswa kujua kwamba ukiwa na tunda hili nyumbani, basi utanufaika kwa njia tofauti.

Katika masuala ya urembo, maji ya ndimu hutumika kwa njia zifuatazo:

Kuimarisha rangi ya ngozi

Changanya kijiko kimoja cha chai cha maji ya ndimu na vikombe viwili vya maji. Ukitumia pamba au kitambaa pangusa uso wako na ukae kwa dakika 20 kabla ya kusuuza. Asidi halisi kwenye siki itachochea mzunguko wa damu katika sehemu hii, vile vile kupunguza vinyweleo.

Kutuliza ngozi

Changanya maji ya ndimu maji moto ya kuoga kisha ukae ndani kwa dakika 15. Kutokana na sababu kuwa kiwango cha pH cha maji ya ndimu ni sawa na kiwango cha safu inayolinda ngozi yako, hii itakusaidia kuimarisha usawa.

Kusafisha nywele

Changanya vijiko viwili vya chai vya maji ya ndimu na kikombe kimoja cha maji na utumie mchanganyiko huo kusuuza nywele zako. Asidi kwenye maji ya ndimu huondoa masalio ya bidhaa za nywele zilizorundika kwenye nywele zako na hivyo kuzifanya zing’ae.

Utulivu wa miyale ya jua

Changanya kikombe 1/2 cha maji ya ndimu na vikombe vinne vya maji kisha utumbukize kitambaa mle ndani na utumie kupangusa maeneo yaliyochomeka kutokana na miyale ya jua. Maji ya ndimu husaidia kurejesha usawa wa kiwango cha pH kwenye ngozi yako na kuzuia malengelenge.

Kukabiliana na uvimbe baada ya kunyoa nywele

Lowesha pamba kwenye maji ya ndimu ambayo hayajachanganywa na maji, kisha upanguuze maeneo yaliyo na uvimbe huu na uache kwa dakika tano kabla ya kusuuza kwa maji safi na kukausha.

Kitulizo cha mba

Changanya viwango sawa vya maji ya ndimu na maji kisha utumie mchanganyiko huu kusugua ngozi ya kichwa na nywele zake. Pia waweza changanya kijiiko cha chai cha maji ya ndimu kwenye shampoo yako ya kawaida na utumie kuosha nywele zako.

Kuondoa harufu mbaya makwapani

Juisi ya ndimu ina asidi ya citric inayoangamiza bakteria zinazopatikana kwenye makwapa. Lakini hata unapofanya hivi, unashauriwa kutokuwa na mazoea ya kutumia bidhaa hii makwapani kwani yaweza sababisha mwasho kwenye ngozi hasa wakati wa jua.