Habari

Faili ya diwani wa picha ya Ruto akiwa amevalia kijeshi yawasilishwa kwa DPP

June 4th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

FAILI ya kesi ya Diwani (MCA) wa Witeithie, Juja kuhusu uchoraji wa picha ya Naibu Rais kwenye gari lake la matatu imewasilishwa mbele ya mkuu wa mashtaka DPP ili kufanyiwa uchunguzi zaidi.

Kiongozi wa Mashtaka wa Mahakama ya Thika, Bw Kirongo Muitwa, ameambia mahakama kuwa baada ya afisi ya upelelezi Juja kufanya uchunguzi wake kwa siku tano ilizopewa hapo awali, wamewasilisha faili hiyo mbele ya afisi ya DPP, Nairobi kwa uchunguzi zaidi.

“Ningetaka Mahakama ipewe muda wa wiki mbili ili afisi ya DPP ifanye uchunguzi wake kuhusu mwelekeo wa kesi hiyo,” amesema Bw Muitwa wakati Diwani Julius Macharia alifikishwa tena mahakamani mapema Jumanne.

MCA wa wadi ya Witeithie, Juja Bw Julius ‘Taki’ Macharia (mwenye shati jekundu) akiwa na wakili wake Bw Ishmael Nguring’a (katikati) baada ya faili yake kuwasilishwa kwa afisi ya DPP Juni 4, 2019. Picha/ Lawrence Ongaro

Mashtaka dhidi ya MCA huyo ni kwamba mnamo Mei 27, 2019, katika eneo la Juja maafisa wa trafiki walipata gari lake la matatu likiwa limechorwa picha ya Naibu Rais akiwa na magwanda ya kijeshi kama Amiri Jeshi Mkuu.

Hakimu wa Thika Bi Kyanya Nyamori, amekubaliana na ombi hilo la kiongozi wa mashtaka akisema atafuata maagizo hayo ili kungoja mwelekeo wa kesi hiyo baada ya kupokea faili hiyo kutoka kwa afisi ya DPP.

Naye wakili wa MCA huyo Bw Ishmael Nguring’a, amesema hana pingamizi yoyote kuhusu ombi hilo huku diwani huyo akiachiliwa kuwa nje akingoja kesi hiyo mnamo Juni 18, 2019.

Diwani huyo amekuwa akizuiliwa kwenye seli za kituo cha polisi cha Juja kwa siku tano.

Wafuasi wake walifurika katika mahakama hiyo huku wengi wao wakitaka kumsabahi baada ya kesi hiyo kuahirishwa tena.

Bw Macharia alionekana mtulivu akiwa kizimbani huku akisikiza maelezo hayo kwa makini.

Baada ya kutoka nje ya mahakama alipata nafasi ya kuzungumza na wafuasi wake huku akisema “yote nimeachia Mungu.”

Kwa muda wa siku tano alipokuwa katika seli za polisi Juja, wafuasi wake wamekuwa wakizuru huko kumjulia hali na hata mapema Jumanne wakaonyesha ushirikiano wao kumtakia mema.