Michezo

FAINALI AFCON: Je, Senegal itaweza kulipiza kisasi dhidi ya Algeria?

July 18th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

CAIRO, MISRI

KIUNGO Badou Ndiaye wa Senegal amewataka vijana wenzake kujituma vilivyo na kunyanyua ubingwa wa Kombe la Afrika (AFCON) mwaka huu ili iwe zawadi murua kwa beki wao mahiri Kalidou Koulibaly atakayekosa kuinogesha fainali hiyo.

Koulibaly ambaye huchezea Napoli nchini Italia hatakuwa sehemu ya kikosi cha Senegal kitakachovaana na Algeria mnamo Ijumaa baada ya kuonyeshwa kadi mbili za manjano kutokana na mechi tatu zilizopita.

Kulingana na Ndiaye ambaye pia amewataka Senegal kulipiza kisasi dhidi ya Algeria, kutokuwapo kwa Ndiaye kambini mwao ni pigo kubwa kwa kocha Aliou Cisse ambaye ameongoza kikosi chake kutinga fainali ya AFCON kwa mara ya kwanza tangu 2002.

“Yasikitisha kwamba Koulibaly hatacheza fainali. Hili ni jambo ambalo litatupa hamasa hata zaidi. Tutacheza kwa lengo la kumshindia taji hili,” akasema Ndiaye.

Huku Senegal wakiwania ufalme wa AFCON kwa mara ya kwanza katika historia, Algeria watakuwa wakitafuta ufalme wa kivumbi hicho kwa mara ya pili baada ya kutawazwa mabingwa mnamo 1990.

Kocha Djamel Belmadi wa Algeria amesema kwa sasa hawezi kabisa kuwaahidi mashabiki wa kikosi chake ubingwa wa AFCON licha ya Desert Foxes kupigiwa upatu wa kutawazwa wafalme.

Mahrez ambaye huwachezea Manchester City nchini Uingereza, amesema kuwa Algeria wana kila sababu ya kuwazima Senegal katika fainali ya Julai 19 na kutawazwa mabingwa wa AFCON mwaka huu.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 aliwafungia Algeria bao la mwisho katika ushindi wa 2-1 waliousajili dhidi ya Nigeria kwenye nusu-fainali ya pili iliyowakutanisha uwanjani Cairo wikendi iliyopita.

 

Fowadi Riyad Mahrez (kushoto) wa Algeria awania mpira dhidi ya Sadio Mane wa Senegal Juni 27, 2019, uwanjani June 30 jijini Cairo. Picha/ AFP

Bao la kwanza la Algeria ambao wanasaka ubingwa wa pili wa AFCON tangu mwaka 1990, lilichangiwa na kosa la beki William Troost-Ekong aliyejifunga kwa upande wa Nigeria katika dakika ya 40.

Japo Odion Ighalo aliwarejesha Nigeria mchezoni kupitia penalti ya dakika ya 72, Mahrez aliyazima ghafla matumaini ya mabingwa hao mara tatu wa AFCON mwishoni mwa kipindi cha pili.

Pigo kubwa zaidi kwa Senegal katika mchuano huo ni ulazima wa kukosa huduma za beki wa Napoli, Kalidou Koulibaly ambaye ameonyeshwa kadi tatu za manjano katika michuano mitatu iliyopita.

“Afueni kubwa zaidi baada ya kuwabwaga Nigeria ni kwamba fainali itatukutanisha na mpinzani tunayemfahamu vyema,” akasema Mahrez.

Algeria ambao hawajapoteza mchuano wowote hadi kufikia sasa kwenye AFCON 2019, walianza kampeni zao za Kundi C kwa kuwabamiza Kenya 2-0, kisha kuwalaza Senegal 1-0 na kuwapepeta Tanzania 3-0.

Jumatano ilikuwa zamu ya Tunisia na Nigeria waliobanduliwa kwenye nusu-fainali kuwania medali ya shaba.

Nigeria ilishinda kwa 1-0 na hivyo kumaliza katika nambari ya tatu AFCON 2019.