Michezo

FAINALI KALI: Algeria na Senegal kukwaana leo Ijumaa

July 19th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

CAIRO, Misri

MBIVU na mbichi kwenye makala ya 32 ya Kombe la Afrika itajulikana leo nchini Misri wakati Teranga Lions ya Senegal na Desert Foxes ya Algeria zitamenyana katika fainali kufunga mashindano haya ya siku 29.

Kundi C, ambalo lilikuwa na Harambee Stars ya Kenya na Taifa Stars ya Tanzania, lilitoa timu hizi zilizofika fainali.

Mabingwa wa mwaka 1990 Algeria wanajivunia kuwa na wachezaji wakali kama Riyad Mahrez (Manchester City), Islam Slimani (Leicester), Sofiane Feghouli (Galatasaray) na Yacine Brahimi (Porto), miongoni mwa wengine. Hawajashindwa katika makala haya ya kwanza kuwa na timu 24. Rekodi hiyo itakuwa hatarini kuvunjwa.

Vijana wa kocha Djamel Belmadi walichapa Kenya 2-0, Senegal 1-0 na Tanzania 3-0 katika mechi za makundi kabla ya kupiga Guinea (3-0), Ivory Coast kwa njia ya penalti 4-3 na Nigeria 2-1 katika raundi ya 16-bora, robo-fainali na nusu-fainali, mtawalia.

Makali yake yatapimwa na Senegal itakayotafuta kulipiza kisasi baada ya kucharazwa na Waalgeria hawa mara nne pamoja na kutoka sare mechi moja katika mechi tano zilizopita.

Vijana wa kocha Aliou Cisse, ambaye alizaliwa siku moja kabla ya Belmadi mnamo Machi 24 mwaka 1976, walilemea Tanzania 2-0 na Kenya 3-0 katika mechi zingine za makundi kabla ya kubandua nje Uganda, Benin na Tunisia katika awamu tatu zilizofuata kwa kuwapiga 1-0 kila mmoja.

Senegal ni nambari moja barani Afrika na 22 katika viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). Algeria ni 12 barani Afrika na 68 duniani.

Teranga Lions ina wachezaji wakali kama Sadio Mane (Liverpool), Keita Balde (Inter Milan), Cheikhou Kouyate (Crystal Palace), Idrissa Gueye (Everton) na Kalidou Koulibaly (Napoli), miongoni mwa wengine.

Hata hivyo, Cisse atakuwa bila Koulibaly katika safu ya ulinzi baada ya kulishwa kadi ya njano dhidi ya Uganda na pia Tunisia. Koulibaly anatumikia marufuku ya mechi moja.

Katika mahojiano na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kabla ya mchuano huo ambao mshindi atatunukiwa Sh463.9 milioni, Cisse alisema Teranga Lions inaheshimu Algeria.

Kocha wa Senegal Aliou Cisse. Picha/ AFP

“Kufika fainali kwetu ni kitu cha kujivunia sana. Algeria ni timu kali na tunawaheshimu. Mechi itakuwa ngumu na bila shaka, tunataka ushindi,” alisema Cisse, ambaye alipoteza penalti akiwa mchezaji katika timu ya Senegal iliyofika fainali na kupigwa na Cameroon kwa njia ya penalti 3-2 mwaka 2002.

Ni mara ya kwanza Senegal imefika fainali tena tangu mwaka huo.

Mchezaji matata Krepin Diatta pia alizungumza na CAF na kusema, “Akili zetu zote ziko katika fainali hiyo. Tutajaribu kadri ya uwezo wetu kuhakikisha tunarejea Senegal na taji.”

Belmadi alisema lengo lao ni hilo la kunyakua taji.

Hata hivyo, alikiri mechi itakuwa ngumu “kutokana na mechi ya mwisho walipokutana.”

“Itakuwa changamoto tofauti, lakini hatuna wasiwasi wowote,” alisema Belmadi, ambaye hatarajiwi kubadilisha kikosi kilichozima Nigeria katika nusu-fainali.

Nambari mbili atajiliwaza na zawadi ya Sh257.5 milioni.