Michezo

Fainali ya UEFA ni Agosti 29

April 19th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

VINARA wa soka ya bara Ulaya, Uefa, wamefichua uwezekano wa kusakatwa kwa fainali ya kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika msimu huu wa 2019-20 mnamo Agosti 29.

Waendeshaji wa kipute hicho wameratibiwa kukutana mnamo Aprili 23 ili kujadili mustakabali wa mechi zilizosalia katika kalenda ya muhula huu ambayo imeathiriwa pakubwa na virusi vya homa kali ya corona.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, huenda waandalizi wa UEFA wakaafikiana kuendelezwa kwa kinyang’anyiro hicho baada ya Ligi Kuu tano za bara Ulaya; yaani EPL (Uingereza), Bundesliga (Ujerumani), La Liga (Uhispania), Serie A (Italia) na Ligue (Ufaransa) kutamatika rasmi.

“Kubwa zaidi kwa sasa ni kuona jinsi ambavyo kampeni zote za Europa League na UEFA msimu huu zitakavyotamatika kufikia mwisho wa Agosti 2020,” akasema Rais wa mashindano hayo ya bara Ulaya, Aleksander Ceferin.

Awali, kinara huyo alikuwa amewapendekezea viongozi wengine wa Uefa kuhusu uwezekano wa mechi hizo kusakatwa ndani ya viwanja vitupu badala ya kuzifutilia mbali kabisa.

Hii ni baada ya washidakau, wakiwemo viongozi wa soka katika mataifa wanachama wa Uefa kutaka vipute vya UEFA na Europa League msimu huu kutupiliwa mbali iwapo virusi vya homa kali ya corona havitakuwa vimedhibitiwa vilivyo kufikia Septemba 2020.

Mapambano ya UEFA na Europa League kwa sasa yamesitishwa kwa muda usiojulikana.

Iwapo mtazamo wa Ceferin utakumbatiwa na wadau wengine katika kikao cha Aprili 23 jijini Paris, Ufaransa, basi huenda fainali ya UEFA ikaandaliwa jijini Istanbul, Uturuki mnamo Agosti 29, siku tatu baada ya kutandazwa kwa fainali ya Europa League jijini Gdansk, Poland.

Hata hivyo, kufanikiwa kwa mipango hiyo kutamaanisha kwamba mikondo miwili ya michuano ya robo-fainali na nusu-fainali itasakatwa kama mechi za kawaida katikati ya ratiba ya Ligi Kuu za mataifa husika wakati wowote kati ya Julai na Agosti.

Namna nyingine itakuwa ni kuandaliwa kwa michuano ya mkondo mmoja pekee katika hatua za robo-fainali na nusu-fainali baada ya kampeni za Ligi Kuu zote tano za bara Ulaya kutamatishwa rasmi mwishoni mwa Julai.

Nne kati ya klabu nane za robo-fainali za UEFA tayari zinajulikana kufikia sasa huku kivumbi cha haiba kati ya Manchester City na Real Madrid kikisalia na mkondo mmoja zaidi kabla ya atakayesonga mbele kujulikana.

Kizungumkuti kikubwa zaidi kipo katika jinsi ya kuratibu mechi za kivumbi cha Europa League kwa sababu michuano yote minane katika hatua ya 16-bora bado haijachezwa huku mechi mbili za mkondo wa kwanza zinazohusiaha klabu za Uhispania na Italia zikiwa bado hazijapigwa.

Vikosi vya Manchester City na Chelsea kutoka Uingereza ndivyo vingalipo katika kivumbi cha UEFA huku Manchester United, Wolves na Rangers kutoka Scotland zikiwa miongoni mwa timu ambazo bado zinawania ufalme wa Europa League muhula huu.

Fainali za UEFA na Europa League kwa upande wa wanawake zilizotarajiwa kufanyika mnamo Mei 2020 tayari zimeahirishwa pia.

Katika mechi nyinginezo za mkondo wa pili wa UEFA, Juventus watavaana na Lyon, Barcelona wapimane ubabe na Napoli nao Bayern Munich wagaragazane na Chelsea.