Michezo

Fainali ya Uefa sasa ni Real Madrid dhidi ya Borussia Dortmund

May 9th, 2024 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

REAL Madrid ilihitaji dakika mbili pekee kuzamisha timu ya FC Bayern Munich kwa mabao 2-1 katika mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (Uefa).

Sasa Madrid ndio itakutana na Borussia Dortmund katika fainali ya dimba hilo.

Dortmund ilikuwa mnamo Jumanne usiku imeizamisha timu ya Paris Saint Germain (PSG) kwa ujumla wa magoli 2-0.

Huku kila hali ikionyesha kwamba timu hizo mbili zilikuwa ziingie kwa muda wa ziada, hali ilibadilika kuwa kiwewe kwa Real Madrid katika dakika ya 68 wakati mchezaji Alphonso Boyle Davies alifungia Bayern goli la kwanza kupitia shuti sawa na mlipuko wa bomu kwa ukali na kasi.

Goli hilo liliifanya Bayern kuwa kifua mbele kwa ujumla wa magoli 3-2 kutokana na hali kwamba timu hizo zilikuwa zimetoka sare ya magoli 2-2 katika mchuano wa awamu ya kwanza ya nusu-fainali yao.

Lakini mambo yalifanyika kwa spidi ya risasi wakati mchezaji Jose Luis Mato Sanmartin (Joselu) alitikisa nyavu za Bayern Munich kunako dakika ya 88 na kabla ya hata mashabiki wake wazalishe mate yaliyokuwa yamekauka wakishangilia goli hilo, akatikisa nyavu tena katika dakika ya 90+1.

Hali hiyo ilimfanya Joselu wa umri wa miaka 34 kutoka Uhispania kuibuka shujaa wa kuwapa furaha mashabiki wake sawa na ya kibogoyo kupata meno ghafla pasipo gharama.

Hapo ndipo bidii ya Joselu ilinyima ligi kuu ya Ujerumani ya Bundesliga nafasi ya kuwakilishwa na timu mbili katika fainali hiyo.