Michezo

Fainali za handiboli ni hapo mwakani

June 6th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Handiboli la Afrika (CAHB) limethibitisha kwamba fainali za kuwania ubingwa wa Kombe la Afrika (AFCON) miongoni mwa wanawake sasa zitaandaliwa mwaka ujao.

Baada ya mapambano mbalimbali katika kalenda mpya iliyotolewa na CAHB kufanyiwa mabadiliko, Shirikisho la Handiboli la Kenya (KHF) limeshikilia kwamba timu ya taifa ya wanawake itashiriki fainali za bara la Afrika zitakazofanyika nchini Cameroon mnamo Juni 11-20, 2021.

Charles Omondi ambaye ni mkurugenzi wa kiufundi wa KHF amesema kwamba macho yao kwa sasa yameelekezwa kwa kipute hicho ambacho kitatoa fursa kwa vikosi sita vya kwanza kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia.

“Vipusa wetu watatuwakilisha katika mashindano hayo ya haiba. Itatulazimu sasa kuanza maandalizi ya mapema ili kuweka hai matumaini ya kufanya vyema,” akasema.

Omondi anaamini kwamba Kenya ina uwezo mkubwa wa kutamba katika mashindano hayo yatakayoleta pamoja timu 16 bora zaidi katika handiboli ya wanawake barani Afrika.

Katika kalenda mpya ya CAHB, vipute sita vimepangiwa kufanyika mwaka huu, kuanzia pambano la Super Cup ambalo mahali na tarehe za kuandaliwa kwalo zitatolewa baadaye mwezi huu.

Mashindano mengine ambayo yameathiriwa ni ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 23 ambayo sasa yataandaliwa nchini Morocco mnamo Disemba 6-12, 2020. Mafunzo yaliyokuwa yahusishe marefa na makocha wa handiboli pia yameahirishwa na tarehe mpya zitatolewa kufikia mwisho wa wiki ijayo.

Mashindano ya kuwania ubingwa wa Winners Cup miongoni mwa klabu za Afrika yaliyokuwa yaandaliwe nchini Algeria sasa yamefutiliwa mbali.

Timu za wanaume za NCPB na Ulinzi zitawakilisha Kenya katika mashindano hayo ya klabu yatakayofanyika nchini Misri mnamo Novemba 13-22, 2020. Nairobi Water watawakilisha vipusa wa Kenya katika mapambano hayo.

KHF imefichua mipango ya kurejelewa kwa mechi za handiboli ya humu nchini pindi baada ya janga la corona kudhibitiwa.