Habari Mseto

Faini ya asilimia 10 ya mamilioni aliyoiba

September 18th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa benki aliyetimuliwa kazini baada ya kuiba Sh2.6milioni miaka mitano iliyopita Alhamisi alitozwa faini ya Sh250,000 ama atumikie kifungo cha mwaka mmoja baada ya kueleza korti amepatwa na misiba mizito tangu ashtakiwe.

Bw Dedan Kamau Nyamathuwe aliomba korti imwonee huruma na isiamuru atumikie kifungo cha jela kwa vile “alifiwa na mama yake mzazi na mtoto wake mtawalia.”

Alisema mikasa hii imemletea msongo wa mawazo na korti ingelimsaidia tu kwa kutomtosa gerezani.

Aliomba hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Bw Francis Andayi “apoze na kutuliza makali ya sheria na huruma na kumpa fursa nyingine kujirekebisha zaidi kwa vile ameghairi matendo yake.”

“Naomba hii mahakama inihurumie. Nimepatwa na misiba mizito mtawalia. Mapema mwaka huu nilifiwa na mama yangu mzazi. Na kama vile wahenga walisema msiba uandamana na mwenziwe-nikafiwa na mtoto wangu,” mshtakiwa alisema

Aliongeza kusema: “Naomba usinifunge gerezani kwa vile maafa yaliyonipata ya kufutwa kazi na kufiwa na mama na mtoto wangu yalifyoza kabisa nguvu za mwili na moyo.Naomba uniruhusu niendelee kushughulikia familia yangu.”

Mshtakiwa aliongeza kusema amejifunza mengi “katika kipindi hiki cha miaka mitano na sitarudia makosa haya tena.”

 “Mshtakiwa yuko na umri wa miaka migapi?” Bw Andayi alimwuliza wakili aliyemwakilisha mshtakiwa.

“Mshtakiwa yuko na umri wa miaka 43,” wakili alijibu.

Hakimu alisema Nyamathuwe aliiba pesa hizo akiwa na umri wa miaka 33.

Bw Andayi alimpata mshtakiwa na hatia ya kuiba Sh2,620,000 kati ya Machi 3 na Oktoba 5 2015 katika tawi la Westlands la Benki ya Co-operative.

Kiongozi wa mashtaka Bi Angela Fuchaka alieleza korti kwamba hana rekodi ya uhalifu ya mshtakiwa na kwamba hatia hiyo ichukuliwe kuwa ya kwanza kufanywa na mshtakiwa.

Bi Fuchaka aliomba korti izingatie kiwango cha pesa benki ilipoteza akipitisha adhabu.

Akipitisha hukumu, hakimu alisema ametilia maanani malilio ya mshtakiwa.

“Unakabiliwa na kosa mbaya la wizi ukiwa mfanyakazi uliyethaminiwa na pesa za wateja lakini ukaiba. Hata hivyo nimetilia maanani malilio yako. Hii mahakama imekutoza faini ya Sh250,000 ama utumikie kifungo cha mwaka mmoja gerezani,” Bw Andayi aliamuru.

Hakimu aliamuru faini hiyo itolewe katika dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu kisha arudishiwe mabaki.