Habari Mseto

Faini ya Sh1.3 milioni kwa kumeza hongo ya Sh50,000

February 7th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wawili wa Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF)  waliolambishwa mlungula wa Sh50,000 na kusema noti zilikuwa na unga wametozwa faini ya Sh1.3 milioni ama watumikie kifungo cha miaka mitatu gerezani.

Bw Kenneth Kipkemoi Settim , aliyepewa kitita cha Sh10,000 na mmiliki wa mkahawa ujulikanao Visa Place alimlalamikia Bw Moses Ngugi Keige pesa hizo zilikuwa na unga unga , lakini akaelezwa “pesa zilipata unga wa kuoka mandazi.”

Bw Settim alizihesabu na kumpa mwenzake Jossy Mwikali Kioko akaziweka ndani ya mkoba aliokuwa amebeba.

Bi Kioko alikuwa amepewa kifurushi cha noti za Sh1,000 zipatazo Sh40,000. Jumla walipokea mlungula wa Sh50,000 wasimshtaki Bw Keige na makosa ya kukataa kuwalipa wafanyakazi Sh3 milioni.

Lakini Settim na Mwikali walikamatwa kabla ya kuondoka hotelini na pesa hizo za unga zikachukuliwa kutoka kwao. Unga huo unaotumiwa kunasa wafisadi pia ulikuwa kwenye mikono yao.

Kisa hicho kilitokea miaka 17 iliyopita na kuifanya kesi hiyo kuwa zee zaidi katika mahakama za kuamua kesi za ufisadi.

Settim na Mwikali walihukumiwa na hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Lawrence Mugambi.

Wawili hao walipatikana na hatia ya makosa mawili ya kudai hongo ya Sh200,000 wasimshtaki Bw Moses Ngugi Keige kwa kukataa kuwalipia wafanyakazi wake ada za NSSF Sh3milioni.

Mahakama iliwapata na hatia pia ya kupokea Sh50,000 kutoka kwa Bw Keige mnamo Julai 23 2002 katika mkahawa wa Visa Place ulioko jijini Nairobi.

Maafisa wa polisi na wale kutoka EACC waliwatia nguvuni washtakiwa katika hoteli ya Visa Place.

Washtakiwa walipewa muda wa siku 14 kukata rufaa ikiwa hawakuridhika na uamuzi huo.