Habari Mseto

Faini ya Sh1,500 kwa kuramba asali hadharani Uhuru Park

May 29th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAUME aliyekamatwa akishiriki ngono hadharani na mwanadada katika bustani ya Uhuru Park, Nairobi alitozwa faini ya Sh1,500 ama atumikie kifungo cha mwezi mmoja gerezani.

Bw Kanara Maina alikiri kushiriki ngono na rafikiye Bi Joyce Wanjiku katika mahala pa umma aliposhtakiwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya City Bi Roselyen Onganyo.

Wawili hao walitiwa nguvuni na askari wa jiji la Nairobi na kushtakiwa kwa kukaidi sheria za kaunti ya jiji la Nairobi.

“Naomba hii mahakama inisamehe,” Maina alijitetea na kuapa mbele ya mahakama “sitarudia kitendo hiki cha aibu tena.”

Bi Onganyo alimwonya vikali na kumwambia “ukirudishwa hapa siku nyingine utaadhibiwa vikali.”

Askari wa jiji walipowakamata wawili hao waliwaachilia kwa dhamana ys Sh500.

Wanjiku hakufika mahakamani kujibu shtaka na hakimu alielezwa “anasakwa kwa vile alikaidi amri afike kortini Jumatano kujibu shtaka.”