Habari Mseto

Faini ya Sh3 milioni mkulima akikataza serikali kukagua shamba lake

March 31st, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

MKULIMA yoyote ambaye anamzuia afisa wa serikali kukagua shamba lake ataadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh3 milioni au afungwe jela kwa miaka mitatu ikiwa sheria mpya za kusimamia kilimo cha mazao ya chakula zitaidhinishwa na bunge.

Sheria hiyo pia inawazuia wakulima kutumia mbolea ya kiasili iliyotengenezwa kwa samadi ya mifugo kukuza mimea ya chakula kama vile mahindi, maharagwe, viatu vitamu, mihogo kati ya mimea mingine ambayo ni tegemeo kuu kwa wananchi wa kawaida.

Kulingana na sheria hizo, ambazo zimetungwa na Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano na Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA), wakulima wa mazao hayo hawataruhusiwa kutumia mbolea ambayo haijaidhinishwa na serikali husika za kaunti.

“Mkulima hataruhusiwa kutumia mbolea ya mifugo kwa ajili ya ukuzaji wa mimea ya chakula, hasa karibu na maeneo ya taka au yenye madini hatari,” sheria hizo zinasema.

Na mazao ya chakula sharti yauzwe katika masoko yaliyoidhinishwa na serikali za kaunti, hali inayoibua maswali ikiwa wakulima wataruhusiwa kuuza mazao hayo kwa majirani wao kama wanavyofanya.

“Wakulima hawaruhusiwi kununua au kuuza mazao kwa watu ambao hawajasajiliwa,” kulingana na sheria hizo.

Na endapo sheria hizo zitapitishwa maafisa wa AFA watakuwa na mamlaka ya kukagua mazao ya chakula katika maghala au hifadhi za kampuni za kutengeneza bidhaa za vyakula. Watakuwa na idhini ya kuharibu bidhaa za chakula ambazo hazijatimiza viwango vya usalama.

Sheria hizo ambazo bado hazijawasilishwa kwa Mkuu wa Sheria kabla ya kupelekwa bungeni, hata hivyo imeibua pingamizi kali miongoni mwa wakulima na kampuni za utengenezaji bidhaa za chakula.

Bw Isaa Chumba ambaye amekuwa akitumia mbolea ya kiasili shambani mwake katika kaunti ya Elgeyo Marakwetu anasema kuwa anapinga sheria hiyo. “Wateja wangu wanapendelea mimea ambayo imekuzwa kwa mbolea ya kiasili. Nikilazimishwa kutumia mbolea ya kisiasa nitapoteza wateja na hivyo kupata hasara,” anasema mkulima huyu ambaye hukuza matunda.