Habari Mseto

Faini ya Sh40,000 kwa kuvuta shisha

July 17th, 2018 1 min read

Na Benson Matheka

WATU kumi na wawili walitozwa faini ya Sh40,000 kila mmoja kwa kupatikana wakivuta Shisha jijini Nairobi.

Watu hao, wengi wao raia wa kigeni, walikamatwa eneo la Kilimani, Nairobi wakihusika na uvutaji wa Shisha kinyume cha sheria. Walikubali mashtaka mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Kibera Elizabeth Osoro ambaye aliwatoza faini ya Sh40, 000 kila mmoja au wafungwe jela miezi sita wakishindwa kulipa faini hiyo.

Mahakama iliambiwa kwamba walipatikana katika maeneo tofauti ya burudani eneo la Kilimani wakivuta Shisha kinyume na sheria za afya ya umma za Kenya.

Upande wa mashtaka ulisema kwamba ilikuwa mara ya kwanza kwa watu hao kushtakiwa na wakachukuliwa kama wakosaji wa kwanza. Mahakama iliwaonya dhidi ya kukiuka sheria.

Katika kesi tofauti mbele ya Hakimu Mkuu Joyce Gandani raia wawili wa kigeni walishtakiwa kwa kupatikana wakifanya kazi nchini bila kibali.

Mahakama iliambiwa kwamba Abdelaziz Abdelaziz na Amr Ahmed Elsayed ambao ni raia wa Misri walipatikana eneo la Langata, Nairobi wakiendesha biashara bila kuwa na kibali kutoka kwa wizara ya uhamiaji ya Kenya.

Walikanusha mashtaka na kuachiliwa kwa mdhamini wa Sh100,000 raia wa Kenya. Kesi itatajwa Julai 31 ili washtakiwa wakabidhiwe taarifa za mashahidi na ushahidi ambao upande wa mashtaka utatengemea katika kesi hiyo.